KENYA WAONDOA VIKWAZO KWA WASAFIRI KUTOKA TANZANIA WALIOCHANJWA CHANJO YA UVIKO-19 KUPIMA TENA UVIKO-19.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Kenya wameingia makubaliano ya kuondoa vikwazo kwa Watanzania wanaoingia nchini Kenya kwa njia ya anga ambapo sasa Watanzania waliochanjwa chanjo ya UVIKO-19 hawatolazimika tena kupima UVIKO-19.
Hayo yamesemwa leo na Mwenyekiti wa Tume ya Pamoja ya Biashara kati ya Tanzania na Kenya ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashana nchini Mhe. Dkt. Ashantu Kijaji kwenye Mkutano wa Saba wa Ngazi ya Mawaziri wa Tume hiyo ya pamoja wakijadili kuhusu utatuzi wa vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiushuru kilichofanyika leo Zanzibar.
Dkt. Ashantu Kijaji, amesema kuwa Serikali ya Kenya imefanyia kazi changamoto iliyowasilishwa na Tanzania na tayari Serikali ya Jamhuri ya Kenya imeondoa sharti lililowekwa kwa Watanzania wanaosafiri kwa njia ya anga licha ya kuchanja chanjo ya UVIKO-19 walilazimika tena kupima kipimo cha ugonjwa wa UVIKO-19.
Katika mkutano wa leo, tume imeweza kufikia muafaka wa kutatua jumla ya vikwazo 10 katika masuala mbalimbali yakiwemo, Biashara, Usafari, Kilimo na Kazi huku vikwazo vingine 15 vikiendelea kujadiliwa ambapo hadi kufikia Mwezi Juni 30 Mwaka 2022 vitakuwa vimetatuliwa.