Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka wadau wa Asasi za Kiraia (NGOs), kuhakikisha kila taasisi inayoanzishwa inatekeleza wajibu wake kwa kuzingatia malengo yaliyobainishwa wakati wa usajili na kwa kuzingatia sheria za nchi.
Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo wakati akifungua mkutano wa Kwanza wa mwaka wa Asasi za Kiraia Zanzibar, huko katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Zanzibar.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Mwinyi aliwataka wasikubali kuona kwamba sifa na malengo mema yaliyopo ya kuanzisha taasisi za kiraia yanatiwa dosari na makundi ya watu wanaojaribu kuanzisha asasi hizo wakiwa na malengo na ajenda za siri au binafsi.
Vilevile, alieleza kwamba wadau hao wanawajibu wa kuhakikisha kwamba mapambano dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma waliyoyaanzisha yanazijumuisha asasi za kiraia.