PROF. MAKUBI AWATAKA WATUMISHI WA WIZARA
AFYA KUFUATA MIONGOZO YA UNUNUZI
Wakurugenzi
wa taasisi na wa Hospitali za rufaa za mikoa wametakiwa kufuata
miongozo na sheria za manunuzi ili kuondoa hati chafu na zenye mashaka
kwenye taasisi zao.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya
afya Prof. Abel Makubi wakati akiendesha mkutano wa baraza kuu la
wafanyakazi wa Wizara ya afya, taasisi pamoja waganga wakuu wa Hospitali
za rufaa za mikoa lililofanyika jijini Dodoma.
Prof. Makubi
amesema ni viongozi wanatakiwa kuwa mfano katika utekelezaji wa majukumu
yao mahali pa kazi kwa kufuata miongozo na sheria ya manunuzi ya bidhaa
kwa ajili ya mahitaji ya ofisi au ujenzi pamoja na maboresho ya
miundombinu ya hospitali zao ili kuondokana na hati chafu au zenye
mashaka.
Aidha, Prof. Makubi aliwataka waganga wafawidhi wa
hospitali za Rufaa za Mikoa kuhakikisha wanasimamia upatikanaji wa
dawa, vifaa na vifaa tiba kwenye hospitali zao.
"Ifike muda kila mgonjwa anayefika kwenye hospitali yako uhakikishe anapata dawa zilizopo kwenye mwongozo wa dawa (STG). Tunataka malalamiko yanayotolewa na wananchi yapungue ikiwemo ukosefu wa dawa pamoja na kutopata huduma kwa wakati". Alisisitiza Prof. Makubi.
Hata hivyo, Katibu Mkuu huyo aliwakumbusha viongozi hao pindi wanaporudi kwenye vituo vyao vya kazi kuwakumbusha madaktari walio chini yao kuandika dawa zilizopo kwenye muongozo huo na wahakikishe dawa wanazoziagiza ni zile ambazo zipo kwenye muongozo.
Prof. Makubi amewataka watumishi hao kutofanya kazi kwa mazoea na wanatakiwa kufanya kazi kulingana na kasi ya utendaji wa viongozi waliopo na kutekeleza majukumu wanayopangiwa kwa weledi.