WAFANYABIASHARA WA MBOLEA
WAONDOLEWA HOFU MIZIGO
KUCHELEWESHWA BANDARINI
Mkurugenzi
wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Dkt. Stephan Ngailo
akiambatana na wafanyabiashara wa mbolea nchini wamekutana na Mkurugenzi
wa Mamlaka ya Bandari nchini (TPA), Eric Hamissi kujadili namna bora ya
kutatua changamoto wanazokutana nazo wafanyabiashara hao nchini.
Kikao
hicho kilifanyika jana tarehe 18 Machi, 2022 katika ukumbi wa
mikutano wa bandari Jijini Dar es Salaam na kufikia mwisho mzuri baada
ya wafanyabiashara kuondolewa wasiwasi wa mizigo yao kuchelewa
kupakuliwa katika bandari hiyo kufuatia juhudi shirikishi baina ya TFRA,
TPA na wafanyabiashara wa mbolea.
Akiwasilisha changamoto za
wafanyabiashara hao, Dkt. Ngailo alisema ni pamoja na ucheleweshwaji wa
kushusha shehena ya mbolea mara inapowasili bandarini, uhaba wa vifaa
kwa ajili ya upakuaji wa shehena za mbolea, ongezeko la gharama
zinazolipwa kwa wamiliki wa meli kutokana na meli zenye shehena ya
mbolea kuchukua muda mrefu kutia nanga na kushusha mzigo.
Aidha,
Dkt. Ngailo alisema changamoto hizo zinapelekea kupanda kwa gharama ya
mbolea pindi zinapowafikia wakulima kutokana gharama kuingizwa kwenye
bei ya mbolea inayowaathiri wakulima.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
wa Mamlaka ya Bandari Tanzania, Erick Hamissi, alisema zipo changamoto
mbalimbali zinazokwamisha utoaji wa mizigo kwa wakati ikiwa ni pamoja
na uwepo wa mvua kwa mwezi Januari uliopelekea baadhi ya mizigo
kutoshushwa kwa kuwa wakati wa mvua zoezi la kushusha aina fulani ya
bidhaa husitishwa pamoja na wafanyabiashara wenyewe kuleta malori
machache ya kubeba mzigo wakati wanapakua mzigo mkubwa .
Pamoja
na hayo, Mkurugenzi Hamissi aliwataka wafanyabiashara hao kuimarisha
mawasiliano baina yao na bandari kwa kutoa taarifa ya mizigo
inayotarajiwa kufika kwa wakati ili utaratibu wa kushusha mizigo hiyo
iwekwe ili kupunguza uchelewevu.
@wizara_ya_kilimo
@bashehussein
@tfra_official
@tpa_tz



