WAZIRI MKUU AKAGUA UJENZI WA NYUMBA ZA WATAKAOHAMA NGORONGORO
Asema Serikali imetenga shilingi bil. 1.2 kwa ajili ya ujenzi huo wilayani Handeni, Tanga
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan Serikali imetenga sh bilioni 1.2 kwa ajili ya awamu ya kwanza ya mradi wa ujenzi wa nyumba za wananchi watakaokubali kwa hiari kuhama katika hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.
Awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mradi huo inahusisha nyumba 103 ambazo zipo katika hatua mbalimbali. Ujenzi ulianza 28 Februari 28, 2022 na hadi kufikia Machi 12, 2022 ujenzi wake umefikia asilimia 78. Nyumba hizo zinajengwa katika kijiji cha Msomera Wilayani Handeni, Tanga.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumapili, Machi 13, 2022) wakati akizungumza na wananchi katika kijiji cha Msomera kabla ya kukagua ujenzi wa nyumba hizo ambazo kati yake nyumba 53 zimepauliwa na hatua za umaliziaji inaendelea, nyumba 42 zipo hatua ya boma na nyumba 8 zipo katika hatua za ujenzi wa msingi.
Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Wizara, Taasisi na Idara zote za Serikali zinazoshughulikia uhamaji wa hiari wa wakazi katika hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kukamilisha zoezi hilo kwa ufanisi.
Waziri Mkuu amesema kuwa wananchi hao waliokubali kuhama kwa hiari licha ya kupewa nyumba na eneo lenye ukubwa wa ekari tatu kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za ufugaji. Wananchi hao wanahama ili shughuli za uhifadhi ziendelee katika eneo hilo.
"Serikali itahakikisha haki zote za binadamu zinazingatiwa katika zoezi hilo la kuwahamisha kwa hiari wananchi wanaoishi kwenye hifadhi ya Ngorongoro kwenda katika maeneo mbalimbali watakayayoyachagua kikiwemo na kijiji hicho cha Msomera, ambapo tayari Serikali imeshapima viwanja 2,500 na kutenga eneo la ekari 1,700 Kwa ajili ya kilimo na malisho”.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewaagiza viongozi wa mkoa wa Tanga wakutane na viongozi wa wa kijiji na wananchi wa eneo hilo ili waendelee kuwaelimisha kuhusu zoezi hilo na umuhimu wake kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla. @owm_tz