Home » » WAZIRI UMMY ATAKA NGUVU IONGEZWE KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA KIFUA KIKUU

WAZIRI UMMY ATAKA NGUVU IONGEZWE KATIKA MAPAMBANO DHIDI YA KIFUA KIKUU

Written By CCMdijitali on Tuesday, March 22, 2022 | March 22, 2022

 





 

WAZIRI UMMY ATAKA NGUVU

 IONGEZWE KATIKA MAPAMBANO 

DHIDI YA KIFUA KIKUU


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka Waganga Wakuu wa Mikoa kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya Kifua Kikuu ikiwemo kuwafikia wagonjwa na kutoa elimu ya ugonjwa huo kwa wananchi.

Waziri Ummy amesema hayo wakati anakabidhi magari manne yatakayoratibu shughuli za Kifua Kikuu kwa Waganga Wakuu pamoja na Makatibu Tawala wa Mikoa ya Shinyanga, Singida, Manyara na Morogoro katika viwanja vya ofisi ndogo za Wizara jijini Dar Es Salaam.

Waziri Ummy amesema magari hayo yamepatikana chini ya udhamini wa Global Fund ambayo yamegharimu Shilingi Milioni 390 na kutaka yakatumike kwa kazi ya Ufuatiliaji na uibuaji wa wagonjwa wa kifua kikuu katika maeneo yaliyokusudiwa.

"Kipaumbele cha magari haya ni kuongeza nguvu ya ufuatiliaji wa wagonjwa ya kifua kikuu lakini tunaweza tukayatumia katika mambo mengine ya shughuli za Afya kwa kuwa wote tunafanya kazi ya kuwahudumia watanzania". Amesema Waziri Ummy.


Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa kifua kikuu 133,000 kila mwaka hali ambayo inahitaji nguvu zaidi katika mapambano.

"Mwaka jana tuliweza kuwafikia wagonjwa 87,000 sawa na asilimia 66, kwahiyo nafurahi kuona tunapiga hatua katika kupambana na ugonjwa huu wa kifua kikuu". Amesema Waziri Ummy.


Aidha, Waziri Ummy ametoa ushauri kwa watanzania endapo mtu ataona dalili za kifua kikuu kujitokeza mapema kupata matibabu kwa kuwa ni bure kwa wote.

Waziri Ummy amebainisha kuwa Kifua kikuu bado kimeendelea kuua watanzania lakini kinatibika ikiwa kitabainika mapema pamoja na kujikinga ikiwa ni njia mojawapo ya kupunguza maambukizi pamoja na vifo.

Tarehe 24 Machi 2022 ni maadhimisho ya Siku ya Kifua Kikuu duniani na yanatarajiwa kufanyika kitaifa Mkoani Tanga.

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link