WAZIRI UMMY ATAKA WATUMISHI WA
AFYA KUBADILI FIKRA KATIKA
UTENDAJI WA KAZI
Waziri
wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amewataka watumishi wa umma katika sekta ya
afya kubadili fikra za utendaji kazi na kuwa wabunifu katika kutatua
changamoto ili kuongeza chachu ya kufikia malengo na kutoa huduma bora
kwa wananchi.
Waziri Ummy amesema hayo leo wakati akifungua
mkutano wa baraza kuu la wafanyakazi wa Wizara ya afya,hospitali za
rufaa za mikoa pamoja na taasisi zilizo chini yake uliofanyika jijini
Dodoma.
“Nitoe rai kwa watumishi wote kubadili fikra zetu katika utendaji na tunatakiwa kufanya kazi kwa bidii tukilenga kufikia malengo na mafanikio tuliyojiwekea. Kila mmoja katika nafasi yake awe mbunifu katika kutatua changamoto zinazomkabili na hatimaye kutoa huduma bora”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy amesema katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan akiwa madarakani ametoa Shilingi bilioni 891.5 kwa ajili ya kuboresha miundombinu pamoja na huduma za afya hivyo amewataka watumishi watumie fursa zinazopatikana zikawe chachu za kupata mafanikio makubwa Zaidi.
Akielezea mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha mwaka mmoja, Waziri Ummy ametaja kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa wajawazito wanaohudhuria kniniki kwa mahudhurio manne na Zaidi, kuimarisha na kuboresha na kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa na ubingwa bobezi, kuimarisha huduma katika Hospitali za rufaa za mikoa.
Kwa upande wa mahusiano na wawekezaji na sekta binafsi, Waziri Ummy amesema sekta binafsi zimesaidia kujenga viwanda vya kuzalisha dawa kupitia makubaliano ya pamoja na wawakilishi wa nchi, mashirika ya kimataifa pamoja na taasisi mbalimbali.
Aidha, mafanikio mengine yaliyopatikana ni pamoja na kuimarisha huduma za uchunguzi wa magonjwa ya milipuko ikiwemo UVIKO-19 kwa kuongeza vipimo vya haraka (Rapid Test) na nija ya vinasaba (RT-PCR). kuimarisha ubora wa takwimu za mifumo kielektroniki ya ugavi wa vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa ngazi zote. Kuboreshwa kwa huduma za maabara na kupata ithibati ya kimataifa.
Kwa upande mwingine Waziri Ummy ameeleza changamoto ambazo bado zinaikabili sekta ya afya ikiwemo utoaji wa huduma bora kwa wananchi hasa wa kipato cha chini.