Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu |
KUCHELEWA KUGUNDUA SARATANI
YATAJWA SABABU INAYOCHANGIA VIFO
KWA ASILIMIA KUBWA
Kuchelewa
kugundua maradhi ya saratani imetajwa kuwa sababu kubwa inayochangia
vifo kutokana na ugonjwa huo kusambaa na kufikia hatua ambayo inakua
ngumu kutibika.
Hayo yamesemwa leo jijini Dar Es Salaam na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi wa ujenzi wa kituo cha cha kisasa cha matibabu ya saratani ambacho kinatekelezwa kwa ubia kati ya Serikali pamoja na Taasisi ya Agha Khan.
Waziri Ummy amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na wagonjwa wapya wa saratani 42,060 kila mwaka ikiwa sawa na wagonjwa 76 katika kila watu 100,000 huku vifo vikiwa ni 29,000 kila mwaka sawa na asilimia 68.
Waziri Ummy amesema wagonjwa wengi wa saratani wanagundulika ugonjwa ukiwa umefika katika hatua ya tatu au ya nne ambayo ni ngumu kutibika huku akitaja sababu ya kuchelewa kugundua saratani ni pamoja na kuwa na vituo vichache vinavyotoa huduma hiyo nchini.
“Kutokana na changamoto ya vituo vichache vya kupima na kutoa matibabu ya saratani nchini, Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeingia ubia na Agha Khan kutekeleza mradi huu ambao utatusaidia kuwafikia watanzania wengi kupata huduma za kupima pamoja na kupata matibabu ya saratani”. Amesema Waziri Ummy.
Waziri Ummy ameongeza kuwa kituo hicho kinatarajia kuhudumia wagonjwa wa saratani takribani 120 kwa siku na hivyo kuweza kuipungua mzigo taasisi ya saratani ya Ocean Road ambayo inahudumia wagonjwa 800 mpaka 900 kwa siku.
Aidha, Waziri Ummy amewataka watanzania kujitokeza mapema na kuwa na utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya zao mara kwa mara ikiwemo saratani.
Waziri Ummy ametaja saratani ambazo zinaongoza nchini ni pamoja na saratani ya mlango wa kizazi kwa wanawake, saratani ya matiti pamoja na saratani ya tezi dume huku maeneo ambayo yanaongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi ni mikoa ya kanda ya mashariki (61%), kanda ya kaskazini (17.3%) na kanda ya ziwa (9.1%).