Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango na mkewe Mama Mbonimpaye Mpango leo tarehe 3 Aprili 2022 wameshiriki Ibada ya Misa Takatifu ya Dominika ya tano ya Kwaresma katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yoseph Jimbo Kuu la Njombe, ibada ilioongozwa na Mhashamu Askofu John Ndimbo.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa ibada hiyo, Makamu wa Rais amewaomba viongozi wa dini na waumini kwa ujumla kuendelea kuliombea taifa pamoja na viongozi wake ili waweze kuongozwa na hekima ya Mungu katika kuwatumikia wananchi. Amewasihi kuendelea kudumisha pamoja na kumuomba mwenyezi Mungu aendelee kuijalia Amani Tanzania.
Aidha Makamu wa Rais amewasihi wananchi wa Njombe na watanzania kwa ujumla kujitokeza katika zoezi la sensa linalotarajiwa kufanyika mwezi agosti mwaka huu. Amesema zoezi hilo litarahisisha utambuzi wa mahitaji na changamoto zinazowakabili wananchi na kurahisisha mipango ya maendeleo.
Makamu wa Rais amewapongeza wananchi wa Mkoa wa Njombe kwa utunzaji na usafi wa mazingira na kuwahimiza kuendelea kulinda na kutunza mazingira mazuri yanaowazunguka.
Mhashamu Askofu John Ndimbo amemshukuru Makamu wa Rais kwa kushiriki ibada hiyo katika kanisa kuu Njombe na kumuhakikishia kwamba kanisa katoliki kwa miaka mitatu limetoa kipaumbele cha pekee katika uhifadhi wa mazingira kwa kuzingatia umuhimu wake kwa maendeleo endelevu.