Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV - Dodoma
ALIYEKUWA
Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Mzee Yusuph Makamba ametoa ya
moyoni kuhusu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia
Suluhu Hassan na Aliyekuwa Katibu Mkuu na Kada mkongwe wa Chama hicho,
Ndugu Abdurahman Kinana.
Mzee Makamba ametoa ya moyoni katika
mkutano Mkuu maalum wa Chama hicho, uliofanyika katika ukumbi wa Jakaya
Kikwete, jijini Dodoma ikiwa baada ya kuugua Macho kwa kipindi cha
miaka miwili. Amesema anaamini baada ya kufariki Hayati Magufuli, nchi
ya Tanzania ipo mikono salama chini ya uongozi wa Mama Samia Suluhu
aliyeshika madaraka kwa sasa.
“Ulivyozungumza na Wanawake wa
Tanzania, nilikusikia ukisema bado hamjachaguliwa Rais Mwanamke katika
taifa hili. Ulisema Rais Mwanamke atachaguliwa mwaka 2025, mimi nasema
Mgombe Mwanamke ni wewe Mama Samia na sio Mwanamke mwengine yeyote”,
amesema Mzee Makamba.
Kuhusu uongozi wa Rais Samia, Mzee Makamba
amesema anaamini ataweza kuliongoza taifa la Tanzania kwa ukamilifu kama
alivyofanya Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete na watangulizi wengine
waliopita katika nafasi hiyo.
“Tumezoea kusema mzigo mzito mpe
Mnyamwezi, lakini hata Mkwere aliwahi kuubeba mzigo huu. Kama Mkwere
amebeba mzigo huu, kwa nini Mzanzibar ashindwe?”, amehoji Mzee Makamba.
“Nyuki
wameingia kwenye Mzinga wa Bibi, na kule visiwani Zanzibar wameingia
kwenye Mzinga wa Babu, sasa tunaona Watanzania wanavyokula Asali kwa
sasa, hii ni kwa sababu ya mambo mazuri yanayofanyika katika Sekta
mbalimbali katika taifa hili la Tanzania”, ameeleza
KUHUSU ABDULRAHMAN KINANA
Mzee
Makamba amesema Chanda chema, huvikwa Pete, amemuasa Katibu Mkuu huyo
wa zamani kumsaidia Rais wa Tanzania kuongoza vyema, akiwa kama msaidizi
wake katika majukumu ya Chama.
“Nakumbuka Ukumbi huu wa Mikutano
ulitakiwa kuitwa jina la Kinana, lakini ukapewa jina la Rais Mstaafu
Jakaya Kikwete. Kumbe Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya Taifa inamtafutia
Umakamu Mwenyekiti wa Chama”, amesema Makamba.
Amesema amefanya
kazi na Kinana katika nyakati tofauti na anamjua vizuri katika utendaji
kazi wake, wakifanya kazi kwenye raha na shida kuhakikisha maendeleo ya
Chama yanapatikana na taifa kwa ujumla.
“Tuliwahi kufikishwa
kwenye Kamati Maadili ya Chama, nakumbuka tukasamehewa wote wawili, na
wewe Kinana samehe yameisha hayo, watu dhaifu hawawezi kusamehe”.