Waumini wa Masjid Arafa Mombasa wakimsikiliza kwa makini Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati akisalimiana nao baada ya Sala ya Ijumaa.
|
Waumini wa Dini ya Kiislamu wametakiwa kuendelea kuiombea Dua Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili iweze kukamilisha azma ya kuwatumikia wananchi wake.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla ametoa kauli hiyo alipokuwa akiwasalimia waumini wa Masjid Arafa Mombasa alipojumuika nao katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.
Amesema katika Ibada zilizotiliwa mkazo hasa katika kipindi hichi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ni suala zima la kuomba Dua hivyo amewataka waumini hao na wananchi kwa ujumla kumuombea Dua Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajji Dkt Hussein Ali Mwinyi aweze kutimiza ahadi zake alizozitoa wakati akiomba ridhaa ya Wazanzibari.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imedhamiria kufanya mengi mazuri kwa maslahi ya wananchi wake akitolea mfano suala la kupunguza gharama katika bidhaa za vyakula ili wananchi wapate nafuu katika kupata huduma hizo.
Mhe. Hemed amewasihi wamuni hao kuunga mkono juhudi hizo hasa kuoneana huruma baina yao kwa kuwasaidia wenye mahitaji na kuwa wepesi kutoa sadaka kuwapa maskini na makundi maalum wakiwemo mayatima, wajane na watu wenye ulemavu.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameendelea kuwakumbusha waumini hao kusimamia mafundisho ya Dini ya Kiislamu kwa kutumia Misikiti kuwafunza watoto maadili mema ili kuja kuwa maimamu bora kwa kuendeleza Dini kwa siku zijazo.
Pamoja na hayo Alhajj Hemed amesisitiza wananchi kushikamana kwa pamoja kuondoa matendo maovu yaliyokithiri katika jamii hasa kuzingatia mafunzo waliyoyapata katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Akitoa Khutba Mskitini hapo Sheikh Said Yunus amewakumbusha waumini hao kujiandaa kufanya mema zaidi katika kumi la Mwisho la Mwezi Mtukufu wa Ramadhan akitolea mfano mwenendo wa Mtume Muhammad (S.A.W) alikuwa akihuwisha kumi la mwisho la Ramadhani kwa kufanya Ibada na kuwaamsha watu wake wa Nyumbani ili kutumia kumi hilo kwa kufanya mambo ya kheri.
Aidha ametumia fursa hiyo kuwataka waumini kuwaendeleza vijana waliohifadhi Qur-an ili kupata jamii yenye kushika kitabu hicho kitukufu.
………………………
Abdulrahim Khamis
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
22/04/2022