Na Shamimu Nyaki - WUSM
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul amesema wizara imetengewa takriban Shilingi Bilioni 2 kwa ajili ya kuboresha miondombinu kwa shule maalumu 56 za michezo.
Mhe. Gekul amesema hayo Agosti 04, 2022 katika Ufunguzi wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA uliofanywa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kasssim Majaliwa katika Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi Tabora.
"Sekta ya Michezo inaendelea kukua, na hii ni kutokana na ushirikiano mnaoutoa nyinyi Viongozi wetu wa juu ambao umesaidia kuibua na kukuza vipaji vya wananmichezo", amesema Mhe. Gekul.
Ameeleza kuwa, Serikali inaendelea kuzalisha wataalamu wa michezo kupitia Vyuo vya Michezo ikiwemo Chuo cha Michezo Malya ambao inawatumia katika kufundisha michezo kwa vijana.
Mhe. Gekul ameongeza kuwa, tayari Mikoa saba imeteuliwa kuanza kuboreshewa miundombinu ya michezo ambapo kiasi ha Shilingi Bilioni 10 zimetengwa na zimeanza kufanya kazi hiyo.
Aidha, Mhe. Gekul amesema Tanzania inaendelea kufanya vizuri katika michezo ambapo katika Michezo ya Jumuiya inayoendelea Birmingham Uingereza, …tayari imechukua Medali ya Fedha katika mchezo wa Riadha huku Mabondia wawili wakitinga hatua ya nusu fainali katika michezo hiyo.
Mwisho