Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema wizara hiyo imebuni Kampeni maarufu kwa sasa nchini ya SensaBika ambayo lengo lake ni kuhamasisha wananchi kushiriki Sensa ya Watu na Makazi mwaka huu 2022.
Dkt. Abbasi ameeleza hayo Agosti 04, 2022 Tabora katika Ufunguzi wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA ambapo amesema kuwa, wizara hiyo ndio nguvu shawishi ya Taifa pamoja na kutoa furaha kwa watanzania, imeanzisha Kampeni hiyo kutokana na wadau wake wengi kuwa na ushawishi katika jamii ambao wataweza kuhamasisha watanzania kushiriki zoezi la Sensa.
"Sisi ni wizara ya kutoa furaha na kupitia sekta zetu tuna wadau wengi ambao wakitumia Kampeni hii kupitia umaarufu na ushawishi walionao kwenye jamii itarahisisha kufikisha ujumbe kwa haraka zaidi kwa jamii kushiriki Sensa", amesema Dkt. Abbasi.
Dkt. Abbasi ametumia nafasi hiyo kumuongoza Mgeni Rasmi, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa pamoja na Viongozi, Wanamichezo na Wananchi waliohudhuria ufunguzi huo kucheza kibwagizo maarufu sana nchini cha SensaBika.