Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam ACP Jumanne Muliro leo tarehe 18 Septemba 2022 amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es salaam linaendelea kusimamia operesheni kali dhidi ya vikundi vinavyojihusisha na uhalifu katika maeneo mbambali ya jiji la Dar es Salaam.
Katika hatua hiyo tarehe 17 Septemba 2022 majira ya saa 22:15 (nne na dakika kumi na tano usiku) huko eneo la “Makongo area 4”, wahalifu 6 sugu wa unyang’anyi wa kutumia silaha (mapanga) walijeruhiwa vibaya na baadae kupoteza maisha baada ya kuwahishwa hospitali kwa matibabu. Tukio hilo limetokea baada ya Polisi kupata taarifa fiche kutoka kwa wananchi wema kuwa kulikuwepo na kundi la wahalifu wapatao 9 waliokuwa tayari katika gari aina ya Toyota Noah yenye namba za usajili T 260 BEP wanatokea maeneo ya Mabibo huku tayari wakiwa na mapanga na zana zingine za kuvunjia na kufanyia uhalifu wanaelekea maeneo ya Goba Kinzudi, Wilaya ya Ubungo kwa lengo la kufanya tukio kubwa la uvamizi wa nyumba kadhaa na kupora mali usiku huo.
Ufuatiliaji wa haraka ulianza na Askari Polisi walipofika eneo la Makongo walikutana na gari hiyo na walipolizuia ili kuwakamata wahalifu hao, walishuka na kuanza kuwatishia kwa mapanga askari Polisi wakikaidi kukamatwa na katika mazingira hayo askari walijihami kwa kufyatua risasi kadhaa hewani lakini wahalifu hao waliendelea kukaidi na kutaka kuwajeruhi Polisi, ndipo walishambuliwa, kujeruhiwa na baadae walipelekwa haraka hospitali lakini kwa bahati mbaya walipoteza maisha. Wahalifu watatu katika purukushani hizo walifanikiwa kukimbia na Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linawasaka na litawakamata haraka iwezekanavyo.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa watu wawili kati ya wahalifu hao ni viongozi wa kundi hilo na wametambuliwa kwa majina ya Salum Juma Mkwama@babu salum anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 27-30 mkazi wa Mbagala na Khalifan@ Khalifa mkazi wa Buguruni, waliwahi kushtakiwa kwa kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha (mapanga) 2021 na baadae kuachiwa kwa sababu mbalimbali za kisheria.
Watuhumiwa hao walikutwa wakiwa na mapanga sita, visu viwili na vifaa vingine vya kuvunjia nyumba.