Na. WAF - Mtwara.
Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imelenga kugawa vyandarua vyenye dawa kwenye kaya mbalimbali katika Mkoa wa Lindi na Mtwara
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas katika uzinduzi wa kampeni ya ugawaji wa vyandarua vyenye dawa kwenye kaya uliofanyika leo Septemba 15, 2022 katika wilaya ya Newala mkoani Mtwara
Kanali Abbas amesema kampeni hii itagawa jumla ya vyandarua 812,118 vyenye dawa katika Halmashauri Sita ambazo zitatoka katika Mikoa miwili ya Mtwara na Lindi
“Halmashauri za Mtwara, Masasi na Nanyumbu kutoka Mkoa wa Mtwara zitapatiwa jumla ya vyandarua 424,711 huku Halmashauri za Mkoa wa Lindi za Mtama, Nachingwea na Ruangwa zitapatiwa vyandarua 387,407.” Amesema Kanali Abbas
Aidha Kanali Abbas ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanatumia vyandarua hivyo watakavyo pewa kwa kujikinga na Malaria na sio vinginevyo.
“Hapa naomba nisisitizie sana kila mwananchi ahakikishe chandarua atakachopatiwa anakitumia kwa ajili ya kujikinga na maambukizi ya Malaria na sio matumizi mengine. Amesema Kanali Abbas
Pia, Kanali Abbas amesema idadi ya vifo vitokanavyo na Malaria vimepungua kwa asilimia 70 kutoka vifo 6,311 mwaka 2015 hadi vifo 1,909 mwaka 2021 Kwa Mkoa wa Mtwara.
MWISHO