Na Englibert Kayombo – WAF, Mwanza.
Imebainishwa kuwa Ugonjwa wa Saratani nchini Tanzania umeendelea kukua kwa kasi huku pia ukisababisha vifo vya watu wengi duniani hivyo ni muhimu elimu juu ya ugonjwa huo iendele kutolewa zaidi ndani ya jamii kujikinga dhidi ya magonjwa hayo yasiyoambukiza.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. @dr_philip_isdor_mpango mapema leo mara baada ya kuzundua Jengo la Huduma za Saratani katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.
“Kwa sasa takwimu zinaonyesha hapa nchini kila mwaka takribani watu 42,000 hupata ugonjwa wa Saratani hii ni idadi kubwa na ndio maana Serikali imeamua kwa dhati kuongeza mapambano dhidi ya ugonjwa huu na magonjwa mengine yasiyoambukiza” amesema Makamu wa Rais Dkt. Mpango.
Amesema Serikali imewekeza na kutekeleza afua mbalimbali za kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo pia mkakati wa kupunguza vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza kwa kutoa elimu zaidi ndani ya jamii kuchukua hatua stahiki za kuboresha mtindo wa maisha, kuzingatia ulaji unaofaa, kupunguza matumizi ya pombe, kuacha matumizi ya tumbaku, kufanya mazoezi na kuepukana na tabia bwete.
Dkt. Mpango amewataka wananchi kufanya uchunguzi wa mara kwa mara wa afya ili kubaini mapema hali za afya zao na endapo watakutwa na Saratani katika hatua ya awali basi watapata tiba na kupona kabisa.
Amesema kuwa mwaka 2021, Wanawake 365,164 walifanyiwa uchunguzi na miongoni mwao wanawake 8,762 walibainika kuwa na dalili za awali za Saratani ya Shingo ya Kizazi.
Aidha Dkt. Mpango ameitaka jamii kuachana na dhana potofu kuhusu ugonjwa wa Saratani na kuhusisha ugonjwa huo na ushirikina huku akiiomba wazazi na jamii kwa ujumla kuhamasisha chanjo dhidi Saratani ya Shingo ya Kizazi ambayo inaongoza kwa kuathiri wanawake wengi.
Sanjari na kutoa elimu hiyo, Makamu wa Rais Dkt. Mpango ameupongeza Uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali na kusaidia katika utoaji wa Huduma za kijamii.