Na Eleuteri Mangi,WUSM
Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu Bw. Saidi Yakubu amepokea vikombe ambayo wizara hiyo imepata ushindi katika mashindano ya Shirikisho la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2022 yaliyofanyika kuanzia Oktoba 1-15, 2022 jijini Tanga.
Mapokezi hayo yamefanyika Oktoba 21, 2022 Mtumba jijini Dodoma ambapo timu ya wizara hiyo ni miongoni mwa timu ambazo zimeshiriki vema mashindano ya SHIMIWI na kuwa miongoni mwa timu zilizopata vikombe na medali katika mashindano hayo.
Akipokea vikombe viwili na medali mbili ambazo wizara hiyo imepata Kaimu Katibu Mkuu Bw. Yakubu amesema “Inafurahisha sana tukiwa tunazungumza hivi na vikombe tunavitazama, hili jambo ni jema na linafurahisha sana, spiriti hapa michezo ni upendo, furaha, Amani, kufahamiana na kujenga afya”.
Vikombe ambavyo Wizara hiyo imepata ni cha mshindi wa kwanza kwa mchezo wa karata ambapo Sudi Juma ni bingwa wa mchezo huo, kikobe cha pili ni cha mshindi wa tatu katika mchezo wa drafti ambapo Juma Mohamed ndiye ameikwakilisha vema Wizara katika mashindano hayo na hivyo kuifanya wizara hiyo kuwa na makombe hayo.
Aidha, katika mchezo wa riadha, mwanaridha Anita Brown ndiye aling’ara katika mbio za mita 100 na 200 wanawake kwa kuwa mshindi kwa kushika nafasi ya kwanza katika mbio hizo ambazo zilitimua vumbi katika kiwanja cha shule ya Sekondari ya Ufundi Tanga.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Utamaduni Sports Club Bi. Ester Mnyuku michezo ambayo wizara hiyo imefanya vizuri kuwa ni karata, draft pamoja na riadha. Michezo ambayo wizara hiyo imeshiriki kwa ujumla wake katika mashindano hayo ni Netiboli, Kamba wanaume, riadha, bao, karata, draft.
Kwa upande wake Mkuu wa msafara wa timu hiyo ambaye pia ni Mkurugenzi Msaidizi Utawala Bw, Gideon Malabeja amesema wizara hiyo imeshiriki vema mashindano ya SHIMIWI jijini Tanga ambapo kikosi chake kilikuwa na wachezaji 45 ambao walishiriki mashindano hayo na kurudi salama katika vituo vyao vya kazi.
Mashindano hayo yalianza Oktoba 1-15, 2022 na kufunguliwa rasmi Oktoba 5, 2022 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,Mhe. Jenista Mhagama na kufungwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba Oktoba 15, 2022.