Home » » KAMATI YA MAWAZIRI WIZARA ZA KISEKTA YAANZA ZIARA MIKOA 14 KUTATUA MIGOGORO YA MATUMIZI YA RDHI

KAMATI YA MAWAZIRI WIZARA ZA KISEKTA YAANZA ZIARA MIKOA 14 KUTATUA MIGOGORO YA MATUMIZI YA RDHI

Written By CCMdijitali on Tuesday, October 11, 2022 | October 11, 2022

 

Na Munir Shemweta, WANMM RUKWA

 

 

Mawaziri wa Wizara za Kisekta wameanza ziara ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.

 

Ziara ya Mawaziri hao imeanza leo tarehe 11 Oktoba 2022 katika mkoa wa Rukwa na itaendelea mkoa wa Katavi tarehe 12 Oktoba 2022 kabla ya kuelekea Kigoma Oktoba 13, 2022.

 

Katika mikoa hiyo mitatu ya mwanzo, Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta itaoongozwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Dkt Mashimba Ndaki.

 

Mikoa mingine itakayotembelewa na Kamati hiyo itakayohitmisha ziara yake Oktoba 28, 2022 mkoani Dar es Salaam ni pamoja na Kagera, Mwanza, Simiyu, Shinyanga, Njombe, Iringa, Mbeya, Ruvuma, Lindi na Mtwara.

 

Wakati wa ziara yake, Kamati itakutana na Sekreterieti za mikoa na wilaya na kutoa mrejesho wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 pamoja  na kutembelea baadhi ya maeneo yenye migogoro.

 

Baadhi ya Mapendekezo ya kamati kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi ni kubakisha vijiji na vitongoji vilivyomo ndani ya hifadhi, kubainisha maeneo ya hifadhi yaliyopoteza sifa ili kugawiwa kwa wananchi na kuhakiki pamoja na kurekebisha mipaka kati ya hifadhi za misitu, wanyama na makazi.

 

Pia yapo mapendekezo ya kumega baadhi ya hifadhi na kugawia wafugaji na wakulima, kufanya mapitio ya sheria zinazohusiana na matumizi ya ardhi, kupitia upya sheria ya vyanzo vya maji inayozungumzia mita 60 na kufutwa kwa mashamba yasiyoendelezwa.

 

Tayari timu za wataalamu kutoka wizara za kisekta ziko uwandani katika maeneo mbalimbali ya mikoa hiyo kuhakikisha Kamati ya Mawaziri inafanya kazi yake kwa ufanisi

 

Mawaziri wanaoshiriki ziara hiyo mbali na Mhe Dkt Mashimba Ndaki ni Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Joseph Silinde, Naibu Waziri Maliasili na Utalii Mary Masanja, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Khamis Hamza Chillo na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete.

 


Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Mashimba Ndaki akizungumza katika kikao na viongozi wa mkoa wa Rukwa wakati Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta ilipotembelea mkoa huo kupeleka mrejesho wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 tarehe 11 Oktoba 2022.
Sehemu ya wajumbe wa Sekretarieti ya mkoa wa Rukwa wakifuatilia mrejesho wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 uliotolewa na Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta kwenye mkutano uliofanyika Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Rukwa Oktoba 11, 2022.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Mashimba Ndaki (Katikati) Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete (Kulia), Naibu Waziri TAMISEMI David Silinde na Naibu Waziri Kilimo Anthony Mavunde (Kushoto) wakiteremka kwenye Helikopta wakati wa ziara Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta kushughulikia utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 tarehe 11 Oktoba 2022.

aziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe Mashimba Ndaki (Wa pili kulia), Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Ridhiwani Kikwete (Kulia), Naibu Waziri TAMISEMI David Silinde (Wa pili kushoto) na Naibu Waziri Kilimo Anthony Mavunde (Kushoto) wakiwasili mkoani Rukwa wakati wa ziara Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta kutoa mrejesho wa utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 tarehe 11 Oktoba 2022. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)

 

Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link