Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana na Shirika la Wanawake Duniani katika kuhakikisha wanatimiza malengo yao waliyojiwekea.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa Kauli hiyo alipokutana na Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake (UN Women) Bi Sima Sami Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.
Amesema Umoja wa Mataifa unaendesha Miradi ya Maendeleo katika Sekta mbali mbali ambapo Serikali itaendelea kusimamia Miradi hiyo ili iweze kukamilika.
Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatambua umuhimu wa Wanawake katika Maendeleo ambapo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi amewaamini Wanawake na kuwapa Nyadhifa mbali mbali katika Uongozi ikiwemo Mawaziri na kuongoza Taasisi mbali mbali.
Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amemuhakikishia Katibu Mtendaji huyo kuwa SMZ itaendelea kusimamia mikakati ya Shirika hilo ili kufikia malengo waliojiwekea.
Mhe. Hemed ametumia Fursa hiyo kumuomba Katibu Mtendaji huyo kuandaa utaratibu wa kuwaongezea uzoefu Wanawake wa Zanzibar ili kuendana na kasi ya Dunia kimaendeleo.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake Bi Sima Sami amefurahishwa kuona Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inathamini mchango wa Wanawake kwa kuzingatia uwezo walionao.
Ameeleza kuwa Shirika hilo lina mikakati mingi kwa kuwainua Wanawake na kuiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa Mashirikiano ya kutosha kufikia malengo yao.
ABDULRAHIM KHAMIS
AFISI YA MAKAMU WA PILI WA PILI WA RAIS
13 /10/ 2022