Shamra shamra za Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara za Serikali (SHIMIWI) jijini Tanga zimehamia katika mchezo wa bao kwa wanaume na wanawake.
Mchezo huo umefanyika Oktoba 13, 2022 katika ukumbi wa Bwalo la Maafisa wa Polisi jijini Tanga na kuhudhuriwa na watazamaji lukuki wakishangilia timu zao ili waweze kushika nafasi ya kwanza hadi ya tatu hatua inayowaongezea alama na kupata vikombe vya ushindi.
Haikuwa kazi rahisi kufikia shamra shamra hizo kwa Ofisi ya Makamu wa Rais pamoja na Wizara ya Afya ambapo wachezaji wao wameibuka kidedea na kushika nafasi ya kwanza katika mchezo wa bao licha ya mchezo kuwa mzuri na mgumu kwa kila timu kwa kuwa timu zote zlijipanga na kujiandaa vizuri kwa mashindano hayo.
Kwa upande wa wanawake, bingwa wa mchezo wa bao ni Ofarasia Muhoha kutoka Wizara ya Afya, nafasi ya pili imekwenda kwa Sheila Mabakila na nafasi ya tatu ikachukuliwa na Jamila Kalambo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Aidha, kwa wanaume nafasi ya kwanza imekwenda kwa Jackson Mwakyelu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, mshindi wa pili ni Shamuni Ibrahim kutoka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara wakati nafasi ya tatu imekwenda kwa Hashim Rashid kutoka Idara ya Mahakama Tanzania.
Katika mashindano hayo mchezo wa mpira wa miguu, timu ya Idara ya Mahakama imeingia hatua ya fainali baada ya kuifunga timu ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa penati 5-4 baada kutoka sare ya bila kufungana kwa dakika 90 za mchezo huo uliochezwa katika uwanja wa shule ya Sekondari ya Galanos.
Aidha, katika mchezo mwingine wa nusu fainali, timu ya Hazina ya Wizara ya Fedha na Mipango imeshinda kwa penati 4-3 dhidi ya timu ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (sekta ya Ujenzi) na kuungana na timu ya Idara ya Mahakama ambao watacheza fainali Oktoba 15, 2022 katika uwanja wa Mkwakwani.
Mashindano ya SHIMIWI 2022 ambayo yanatarajiwa kufikia kilele Oktoba 15, 2022 na yanatarajiwa kufungwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba.