Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule, hivi karibuni amesaini mkataba wa utendaji kazi za lishe baina yake, Katibnu Tawala na wakuu wa Wilaya ambao unaratibiwa na kusimamiwa na idara ya afya Mkoa. Shughuli hiyo imefanyika katika ukumbi wa Mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Lengo kubwa la mkataba huu ni kufanikisha suala la kuboresha hali ya lishe na kupunguza athari za utapiamlo katika Halmasahauri, kuhakikisha Halmashauri inasimamia ipasavyo utekelezaji wa afua za lishe pamoja na kuchukua hatua madhubuti za kupunguza hali duni ya lishe katika halmashauri.
Akiongea, mara baada ya kusaini mkataba huo , Mhe.Senyamule amesema kuwa mkataba huo umepewa uzito wa pekee na Serikali ndio maana wamesaini na amewataka wakuu wa Wilaya kwenda kuutekeleza.
“Twende tukaupe uzito mkataba huu na tukautekeleze, tuongeze ufanisi na ubora kwenye hili kwani Dodoma bado tuna tatizo la lishe kwani tunaambiwa udumavu upo kwa asilimia 37 hivyo tuna kazi kubwa ya kufanya kwa ajili ya lishe”
Hata hivyo, Mhe. Senyamule ametoa maelekezo juu ya upandaji miti ya matunda kwani matunda yanasaidia katika kuboresha lishe hasa kwa Watoto.
“Tufanye vikao na tathmini za uhalisia juu ya tatizo la lishe na mukasimamie zoezi la upandaji miti ya matunda ili watoto wapate matunda kwa afya” Amesisitiza Mhe.Senyamule.
Utekelezaji wa mkataba wa utendaji kazi za lishe unasimamia pia utoaji wa taarifa kwani kila Wilaya itatakiwa kuwasilisha taarifa za utendaji kazi za kila robo mwaka kila ifikapo tarehe 07 ya mwezi unaofuata huku taarifa ya utendaji kazi ya mwaka ikitakiwa kuwasilishwa kabla ya tarehe 16 ya mwezi Julai ya kila mwaka.
Aidha, mkataba huu wa kiutendaji utakua wa muda wa miaka nane (8) na umeanza rasmi Julai Mosi, 2022 hadi Juni 30, mwaka 2030 na utakua ukipimwa kila mwisho wa mwaka husika. Iwapo utajitokeza mgogoro wowote katika utekelezaji wake, pande zote mbili zitakaa pamoja ili kutatua mgogoro huo.
MWISHO