Na Munir Shemweta, WANMM SIMIYU
Naibu Waziri wa Kilimo Mh. Anthony Mavunde amesema serikali ipo njiani kutunga sheria maalum kwa ajili ya kilimo ili kulinda maeneo yote yanayofaa kwa kilimo katika azma yake ya kukuza sekta ya kilimo nchini.
Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Ihusi-Bariadi,Mkoani Simiyu katika mkutano wa hadhara wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya Vijiji 975 walipofika katika eneo hilo.
“Katika kulinda maeneo yanayofaa kwa kilimo na kupunguza migogoro ya matumizi ya Ardhi nchini,serikali kupitia wizara ya kilimo tunaendelea na hatua za utungwaji wa sheria ya kilimo.
‘’Kwakuwa dhamira yetu kubwa ni kuhakikisha tunakuza sekta hii ya kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030,hatua hii lazima iende sambamba na kuyatambua maeneo ya kilimo na kuyalinda kisheria’’. Alisema Mavunde
Kwa mujibu wa Mavunde katika maeneo yote ya utatuzi wa migogoro ardhi inamegwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji mali na kutaka mamlaka za upangaji wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo husika kuhakikisha zinatenga maeneo ya mashamba makubwa ya pamoja ya kilimo (block farms) ili serikali iweze kuwahudumia wakulima kwa urahisi.
Katika hatua nyingine,Naibu Waziri Mavunde ametoa rai kwa wakulima wote kuendelea na kukamilisha zoezi la usajili wao ili wanufaike na huduma mbalimbali kutoka serikalini na hasa mbolea ya ruzuku ambapo serikali imetenga zaidi ya Tsh 150 bilioni kama sehemu ya ruzuku ya mbolea ili kumpunguzia mzigo mkulima.
Hatua hiyo inafuatia kupanda kwa bei ya mbolea katika soko la dunia jambo linalowafanya wakulima wa kawaida kushindwa kumudu kununua mbolea na hivyo kuathiri kukua kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo nchini.
Amesema kiasi hicho cha fedha kilichotengwa kitawawezesha wakulima kununua mbolea kwa nusu bei iliyopo kwenye soko.
Naibu Waziri Mavunde alitumia fursa hiyo pia kumshukuru Mh Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza bajeti ya Wizara ya Kilimo kutoka Bilioni 294 hadi Bilioni 954 ambapo Shilingi Bilioni 400 zimeelekezwa kilimo cha umwagiliaji hasa katika kuyafanyia upembuzi yakinifu na usanifu wa kina mabonde yote makubwa nchini sambamba na ujenzi wa mabwawa mapya 13.
----MWISHO-------------
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe
Anthony Mavunde akizungumza na
wananchi wa kata ya Ihusi-Bariadi, Mkoani Simiyu katika mkutano wa hadhara
wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya
Vijiji 975 walipofika katika eneo hilo jana.
Sehemu ya wananchi wa kata ya Ihusi –Bariadi mkoani
Shinyanga wakiwa katika mkutano wa hadhara wakati kamati ya mawaziri 8 wa kisekta
wanaoshughulikia migogoro ya Ardhi ya Vijiji 975 walipofika katika eneo hilo
jana.