Wananchi wa kijiji cha Nambogo Manispaa ya Sumbawanga wameishukuru serikali ya Awamu ya Sita kwa kusaidia kukamilisha ujenzi wa zahanati yao iliyoanza kujengwa mwaka 2000 na kukamilika mwaka huu.
Akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa zahanati hiyo (Novemba 05, 2022) kwa niaba ya wananchi Mzee Lemeli Mbalamwezi (86) ambaye ndiye alitoa eneo hilo alisema wanaishukuru serikali kwa kutoa fedha zilizosaidia mradi huo.
“Tunashukuru viongozi wa chama na serikali kwa kutujengea jengo la zahanati hapa Nambogo na sasa tusaidiwe kupata shule ya sekondari karibu na kijiji chetu”alisema Mzee Mbalamwezi.
Mgeni rasmi kwenye uzinduzi huo, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga alisema alisema anamshukuru Rais Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha pia kumwamini na kumteua kufanya kazi Rukwa ambapo atahakikisha hakuna miradi viporo inasalia.
Sendiga alipongeza pia Manispaa ya Sumbawanga kwa kutekeleza maelekezo yake aliyoyatoa Oktoba 05 mwaka huu alipokagua zahanati hiyo kuwa watoe fedha za mapato ya ndani kukamilisha kazi iliyoanzishwa na wananchi miaka 22 iliyopita.
“Watumishi wenzangu wa serikali mkiniona kwenye maeneo yenu msinune kwani Rukwa bila miradi ya viporo inawezekana. Tusiishi kwa presha, tufanye kazi na kutimiza wajibu wetu wa kuhudumia wananchi “alisisitiza Sendiga.
Akitoa taarifa ya mradi huo Mtendaji wa Kata ya Milanzi, Leonard Nyami alisema mradi huo ulibuliwa na wananchi mwaka 2000 kwa nguvu zao sawa na shilingi Milioni 14.3 kisha serikali mwaka 2021 ilitoa shilingi Milioni 50 na halmashauri mwaka 2022 ilitoa shilingi Milioni 19.
Milanzi aliongeza kusema mradi huo hadi unakamilika mwaka huu umetumia jumla ya shilingi Milioni 87.6 kati ya makisio ya Shilingi Milioni 130 zilizopangwa.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa huyo wa Rukwa ametoa wito kwa wananchi kuendelea kulinda miundombinu ya miradi ya serikali na pia huku ameigiza Manispaa ya Sumbawanga kufikisha huduma ya maji na vifaa tiba kwenye zahanati hiyo.
Mwisho.
@queen__sendiga @wizara_afyatz @ummymwalimu