MKUU wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amewataka wakuu wa Wilaya kuhakikisha wanazingatia mkataba wa lishe ili kupunguza vifo vya watoto wachanga.
Ameyasema hayo Mjini Kibaha kwenye kikao cha kusaini mkataba wa lishe kwa kipindi cha miaka nane hadi Juni 30 mwaka 2030 baina yake na wakuu wa Wilaya za mkoa huo.
Kunenge asema kuwa mkataba huo una malengo ya kupunguza vifo vya watoto wachanga ambapo kupitia mkataba huo faida zitakazopatikana ni kupungua kwa vifo hivyo endapo suala la lishe litazingatiwa.
"Faida nyingine ya kusainiwa mkataba huu ni kuondoa kaya asilimia 1.8 ambazo zinatumia chumvi ambayo haina madini joto ya kutosha, kuhakikisha utapiamlo kwa watoto hauzidi asilimia tano ya viwango vinavyokubalika duniani,"amesema Kunenge.
Aidha amesema kuwa faida nyingine ni kuimarisha mkakati wa mwaka 1994 wa uwekaji madini joto kwenye chumvi kwa ajili ya kuzuia na kudhibiti magonjwa yatokanayo na upungufu wa madini joto mwilini.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani Gunini Kamba amesema kuwa lishe duni ni hatari zaidi kwa wanawake wajawazito, watoto wachanga ambapo athari zake ni vifo kwa akina mama na watoto.
Kamba amesema kuwa lishe duni husababisha kinga ya mwili kushuka na mwili kushindwa kupambana na vimelea vya magonjwa hivyo ni muhimu lishe bora kuzingatiwa kuanzia ngazi ya Kijiji Mtaa na kata na hiyo itasaidia kupunguza gharama za matibabu ambapo watatoa elimu kuhusu lishe bora.