Home » » PROFESA MBARAWA AWATAKA TRC KUTOA TAARIFA KWA WAKATI

PROFESA MBARAWA AWATAKA TRC KUTOA TAARIFA KWA WAKATI

Written By CCMdijitali on Friday, November 25, 2022 | November 25, 2022


PROFESA MBARAWA AWATAKA TRC KUTOA TAARIFA KWA WAKATI
 
Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa amelitaka Shirika la Reli nchini (TRC), kutoa taarifa kwa wakati kuhusu maendeleo ya reli ya kisasa ya sgr na mchakato wa ununuzi na mapokezi ya vifaa vyote vya reli hiyo.
 
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa mapokezi ya mabehewa 14 kati ya 59 ya awamu ya kwanza ya SGR yaliyowasili Prof. Mbarawa amesema zaidi ya shilingi bilioni 882 tayari zimetumika katika kununua vichwa vya treni, mabehewa  na vifaa vingine muhimu vitakavyotumika katika uendeshaji wa reli  hiyo na vitawasili kwa awamu.
 
“Waelezeni wananchi ukweli kuwa kuna mabehewa ya aina tatu yaliyoagizwa yaani daraja la kwanza, la juu na la tatu ili wasipotoshwe pindi yanapowasili”, amesema Prof. Mbarawa.
 
Prof. Mbarawa amesisitiza kuwa mabehewa 45 yaliyosalia ya daraja la tatu yatawasili mwezi mei mwakani. 
 
Amezungumzia umuhimu wa wanahabari kufanya utafiti na kujiridhisha kwa vyanzo sahihi kabla ya kuandika na kutangaza taarifa za miradi mikubwa ya kitaifa ili kuondoa upotoshaji kwa wananchi.
 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Bw.  Masanja Kadogosa amesema wamejipanga kuongeza mabehewa katika reli ya kati na kaskazini katika kipindi cha mwisho wa mwaka ili kuondoa changamoto za usafiri.
 
“Tumejipanga kuhakikisha usafiri wetu unakuwa salama na safari zote zinafuata ratiba iliyopangwa ili kutoa huduma bora kwa wananchi’ amesisitiza Kadogosa.
 
Naye Balozi wa Korea Kusini, Kim Sun Pyo amesema nchi yake itaendeleza ushirikiano na Tanzania katika uimarishaji wa miundombinu nchini. 

@tzrailways






Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link