Wafanyakazi KADCO watakiwa kuwa Wazalendo.
Na Jamal Zuberi, Tanga
Serikali mkoani Tanga imesema kuwa mikutano ya Baraza la Wafanyakazi itumike kujadili malengo na mipango ya Taasisi ikiwa ni pamoja na maslahi ya watumishi.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba akifungua Mkutano wa kwanza 2022/2023 wa Baraza la Wafanyakazi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO) katika ukumbi wa Tanga Beach Hoteli, Jijini Tanga.
"Mabaraza haya ni jukwaa muhimu kujadili utendaji wa kazi wa kila siku na jinsi ya kuboresha utendaji huo zaidi" alisisitiza zaidi Mgumba.
Amesema kuwa ni muhimu tija na maslahi lazima yawe na uwiano ili kuwa na matokeo chanya ya utendaji bora, unaolenga kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi tunaowatumikia.
"Tuelewane utendaji bora zaidi unaongeza tija, tija ikiongezeka ni rahisi kuongeza maslahi ambayo hatimae yanawawezesha watumishi kuishi maisha bora zaidi.
" Naomba kama watumishi katika Sekta ya Usafirishaji wa Anga, lazima mfanye kazi kwa uzalendo, maadili na nidhamu ya juu muonyeshe mfano wakuigwa " alisisitiza Mkuu huyo
Mgumba amewapongeza Wafanyakazi hao wa KADCO kuwa kiwanja bora cha ndege Afirka na Duniani kwa jumla kwa kupewa Tunzo mbali mbali za kimataifa kwa huduma bora pamoja na kuwa na Hati Safi ya matumizi ya fedha.