Home » » RAIS DK.MWINYI ASEMA ZANZIBAR KUWA KIVUTIO CHA KIJANI NA UTALII ENDELEVU

RAIS DK.MWINYI ASEMA ZANZIBAR KUWA KIVUTIO CHA KIJANI NA UTALII ENDELEVU

Written By CCMdijitali on Wednesday, September 27, 2023 | September 27, 2023

 Zanzibar, 


27 Septemba, 2023 


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametoa rai kwa wadau wa kilimo  kuendelea kuliimarisha tamasha la Kilimo Hai liwe kubwa zaidi na endelevu ili kuwavutia watalii. 


Dk. Mwinyi aliyasema hayo alipofungua tamasha la kwanza la Kilimo Hai kwenye viwanja vya maonesho ya kilimo, Kizimbani Mkoa wa Mjini Magharibi. 


Alisema, mwezi Febuari mwaka huu kwenye maadhimisho ya siku ya utalii duniani, Serikali ilizindua azimio la utalii endelevu lililoazimia kuitangaza Zanzibar kuwa kivutio cha kijani na kuzitaka hotel zote za utalii nchini zitumie mazao ya Kilimo Hai na kuweka vyakula vya asili ya Zanzibar. 


Pia alieleza azma ya Serikali kwa hoteli hizo za kitalii kuona uchakataji wa taka unatengenezewa kuwa malighafi endelevu na kutunza mazingira na kuongeza kuwa Serikali haina budi kuendelea kuchukua hatua ya kutimiza asili ya Zanzibar na kuhakikisha watalii wanaokuja Zanzibar wanaendelea kufahamu utamaduni wa Zanzibar. 


Dk. Mwinyi pia alipongeza shughuli za uzalishaji na utengenezaji wa vitu vya asili ikiwemo ufinyanzi wa vyungu, kudarizi vikoi, ushonaji kofia za asili, matumizi ya mapakacha na masusu, mikoba ya ukili na mikeka kwa sehemu kubwa vinaendana na sera ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi na kusaidia kukuza uchumi.

 
Aliongeza, Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo, tayari wamemaliza rasimu ya mikakati ya Kilimo Hai kwa Zanzibar na kueleza maeleza matumai yake ya utekelezaji wa mikakati hiyo, itakuwa suluhisho la changamoto za sekta ya Kilimo Hai inayokabiliana nazo ikiwemo pembejeo za kibaolojia, elimu kwa wakulima na wafugaji pamoja na upatikanaji wa masoko ndani na nje ya nchi. 


Dk. Mwinyi, alibainisha kuwa Serikali inafamu fursa zilizomo ndani ya Kilimo Hai na kueleza dhamira yake endapo mkakati ulioandaliwa ukatengenezewa programu madhubuti na utekelezaji utakaowapa fursa vijana kuanzisha biashara za kutengeneza viatilifu na mbolea hai kwa kusaidia upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi na kuitangaza Zanzibar kama kivutio cha kijani. 


Akizungumzia matumizi ya mbolea za kemikali kwenye utoaji wa elimu kwa watumiaji na walaji, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja ya kuifahamisha jamii kuhusu faida kwenye kuimarisha lishe ili kusaidia kupunguza maradhi yasiyoambukiza kama presha, kisukari na moyo. 


Hata hivyo, alieleza uhalisia wa tamasha hilo unaonekana pia kwenye shughuli nyengine za ujasiriamali. 


Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Kilimo Shamatta Shaame Khamis alieleza azma ya Wizara hiyo inavyoendeleza jitihada za Serikali kushirikiana na taasisi zote zilizomo Zanzibar zinazojishughulisisha na sekta ya kilimo kwa ujumla wake na kueleza mafaniko waliyofikia. 


Alisema, Serikali pia inatoa huduma kwa wakulima wanaozalisha mazao kwa kutumia mbolea za kemikali na kuwapa elimu ya namna bora ya kutumia pamoja na kuishajihisha jamii namna bora ya kutumia viatifu kwaajili ya kuendeleza uzalishaji maalumu. 


Naye, Mwakilishi wa Jimbo la Bububu, Mudrik Ramadhan Soraga alieleza fursa za wanchi wa jimbo hilo hasa kwa Shehia za Dole na Kizimbani wanavyonufaika na fursa za Kilimo Hai na kueleza wanavyojikita kwenye kilimo cha spices na mbogamboga kwa kutumia mbinu bora za kilimo chenye tija kwa afya. 


Mwenyekiti wa taasisi ya Zanzibar Organic Initiativie (ZOI) Dk. Mwatima Abdala Juma alisisitiza haja kwa wakulima na jamii kwa ujumla kuendelea kukiimarisha Kilimo Hai ili kuimarisha afya za watu na afya ya udongo kwa kuepuka matumizi ya mbolea zenye kemikali. 


IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR









Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link