Na Eleuteri Mangi, WUSM, Dar es Salaam
Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Saidi Yakubu amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Kampuni ya Mobi Lottol Tanzania Ltd inayojishughulisha na michezo na michezo ya kubetisha Bw. Deusdedit Mushi ili kujadili namna bora ya kuendeleza sekta ya michezo nchini.
Kikao hicho kimefanyika Septemba 13, 2023 katika Ofisi ndogo za Wizara hiyo jijini Dar es salaam ambacho lengo lake ni kujadili namna bora ya kushirikiana katika kuboresha vipaji vya wanamichezo na miundombinu ya michezo nchini.
“Tumepokea wazo lenu, serikali inawakaribisha kuwekeza katika michezo kufikia malengo ya kuendeleza vipaji vya wanamichezo na miundombinu ya michezo nchini ili kutoa ajira kwa vijana na kuongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla” amesema Katibu Mkuu Bw. Yakubu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Kampuni ya Mobi Lottol Tanzania Bw. Deusdedit Mushi amesema taasisi yao imejikita kwenye kuibua, kutambu na kuendeleza vipaji vya wanamichezo na kuboresha miundombinu ya michezo.