Home » , » TANZANIA NA IRELAND KUSHIRIKIANA KATIKA UTAMADUNI NA MICHEZO

TANZANIA NA IRELAND KUSHIRIKIANA KATIKA UTAMADUNI NA MICHEZO

Written By CCMdijitali on Friday, September 22, 2023 | September 22, 2023


Na Shamimu Nyaki

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amekutana na Balozi wa Ireland hapa nchini Mhe. Mary  O' Neill  na kukukubaliana kushirikiana katika Sekta ya michezo hususan soka la Wanawake pamoja na Sekta ya Sanaa katika eneo la uchoraji.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Septemba 22, 2023 ofisi ndogo za wizara Jijini Dar es Salaam,  Waziri Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amewasilisha ombi kwa nchi hiyo isaidie kutoa mafunzo  kwa Watalaamu wa michezo hapa nchini katika eneo la  usimamizi wa miundombinu ya michezo pamoja na wataalamu wa kufundisha michezo.

"Nawakaribisha katika nchi yetu muweze kufanya maandalizi ya misimu ya ligi zenu kwa kuwa nchi yetu ina maeneo mazuri hapa Dar es Salaam - Kigamboni, Tanga, Arusha na Zanzibar.  
Naamini mtafurahia sana na sasa timu ya Taifa ya Wanawake chini ya Miaka 17 ya nchini Morocco ipo hapa Tanzania ikiwa inacheza mechi za kirafiki na timu yetu ya umri huo" amesisitiza Mhe. Ndumbaro.

Kwa upande wake Balozi huyo Mhe. Mary  O' Neill amekubali maombi hayo na kuahidi kuwa mwezi Novemba mwaka huu atakuja Msanii Nguli  wa fani ya Uchoraji  Mick O'Dea ambaye atatoa uzoefu kwa wasanii wa hapa nchini akibainisha kuwa Wizara  imemkaribisha ashirikiane na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo katika fani hiyo kwakua  ni Taasisi Bora  inayotoa mafunzo kwenye eneo hilo.

Awali Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu ameikaribisha nchi hiyo kupitia Ubalozi huo kushirikiana na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya kutoa mafunzo kwenye fani zinazotolewa chuoni hapo.











Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link