Na Mashaka Mgeta, TANGA
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe Waziri Kindamba, ameahidi kukutana na wazee wa mkoa huo kila baada ya miezi mitatu, ili kujadiliana masuala mbalimbali na kuchangia usuluhishi wa migogoro kwenye jamii.
Mhe. Kindamba ameyasema hayo wakati akizungumza na wajumbe kutoka Taasisi ya Wazee wa Asili wa Wilaya ya Tanga, waliofika ofisini kwake kumkabidhi kitabu cha Mpango wenye lengo la kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakaazi wa jiji la Tanga.
‘’Ninawaahidi kwamba nitakutana nanyi (wazee) kila baada ya miezi mitatu…mambo yatakayonitatiza nitayawasilisha kwenu kwa ushauri ili kupata suluhu ya kudumu ya matatizo yanayotokea kwenye jamii yetu,’’ amesema.
Mhe. Kindamba amesema kitabu kilichowasilishwa na wazee hao kikiwa na kurasa 22, kimesheheni mawazo mema yaliyo kwenye mpangilio mzuri wa kusomeka, kufikirika na kufanyiwa na kazi, hivyo kitatumika katika kuboresha mkakati wa uwekezaji mkoani Tanga, unaotarajiwa kuzinduliwa Novemba mwaka huu.
Kitabu hicho kinazungumzia na kutoa mapendekezo kwa mambo mbalimbali ya kiuchumi ikiwemo bandari, viwanda na changamoto zilizoathiri ukuaji na maendeleo ya sekta hiyo, ardhi, kilimo, uvuvi na uchumi wa bluu, utalii, elimu, afya na miundombinu.
Pia kitabu hicho kina ushauri kwa serikali katika kuandaa mipango ya maendeleo ya uchumi, mazingira, mataraji ya wazee na orodha ya watu mashuhuri wa Tanga waliochangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
@waziriwazirik @owm_tz @maendeleoyajamii @millardayo @matukio_tanga @ccm_dijitali @tanga_jiji @ummymwalimu