Home » » WAZIRI SILAA AANZA NA ENEO LA WAZI DODOMA

WAZIRI SILAA AANZA NA ENEO LA WAZI DODOMA

Written By CCMdijitali on Saturday, September 9, 2023 | September 09, 2023

 WAZIRI SILAA AANZA NA ENEO LA WAZI DODOMA


Na Munir Shemweta, WANMM


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa ameanza kushughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi kwa kukagua eneo la wazi lililopo mtaa wa Surungai eneo la Meriwa kwenye kata ya Ipagala mkoani Dodoma na kusisitiza maeneo ya wazi kuendelea kuwa wazi.

Akiwa katika ziara yake tarehe 8 Septemba 2023 huku akiwa ameambatana na Kamishna wa Ardhi nchini Nathaniel Methew Nhonge, watendaji wa sekta ya ardhi pamoja na watendaji wa Ipagala, Waziri Silaa alijionea namna baadhi ya wananchi walivyovamia eneo la wazi huku baadhi yao wakiwa wamekamilisha ujenzi.

Katika eneo hilo, baadhi ya viongozi wa mitaa wameidhinisha mauziano maeneo ya wazi kienyeji kinyume na michoro ya mipango miji jambo lililosababisha ujenzi kufanyika huku maeneo mengine ujenzi ukiendelea.

‘’Kama huu mchoro ungezingatiwa hapa pangekuwa na mji mzuri na eneo la wazi lingebaki. Wale wananchi wanaoishi na maeneo yao kuwekewa umeme wasibughudhiwe na simamieni maeneo yote yaliyobaki yabaki wazi hapa na maeneo mengine nchi nzima’’ alisema Waziri Silaa

Kwa mujibu wa Waziri huyo wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kiongozi au mtendaji atakayebainika kusaidia wananchi kujenga eneo la wazi basi atawajibika kwa nafasi yake lakini kwa sasa pale ambapo wananchi wamejenga na kuishi basi waendelee kuishi na wasibughudhiwe.

‘’Yale maeneo ya wazi ambayo yako wazi mtu anajenga kiukuta anaeka kibanda na yote yaliyokuwa wazi ama yenye uimarishaji wa muda mfupi au watu wamejitengenezea fensi yote yanatakiwa kuwa wazi ‘’ alisema Silaa.

Ameongeza kuwa, akikuta maeneo hayo ya wazi yamejengwa maana yake kiongozi au mtendaji aliyeruhusu kujengwa atakuwa sehemu ya mgogoro na atachukuliwa hatua.

Aidha, Waziri Silaa ameonya maofisa wa sekta ya ardhi wanaomilikisha wananchi kiwanja kimoja mara mbili (Double allocation) ambapo alieleza kuwa, afisa atakayebainika atawajibika kwa kosa hilo.

‘’ Huyo afisa kama una invoice imetolewa kwenye system ya serikali ina jina la afisa atawajibika moja kwa moja na huo ni ujumbe wa nchi nzima, tukikuta kuna watu wawili wana hati ya kiwanja kimoja ameenda’’ alisema Silaa

 

Mwanzoni mwa wiki hii Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa alielekeza watendaji wa sekta ya ardhi nchini kuhakikisha ndani ya siku mia moja kuanzia sept 4, 2023 wanatatua migogoro ya ardhi kwa kadri ya uwezo wa nafasi zao.

 

Aidha, aliwataka waliovamia maeneo ya wazi kuanza kuondoka mara moja huku akielekeza viongozi na watendaji wa wizara ya ardhi wenye mamlaka ya kusimamia sheria katika maeneo mbalimbali kuhakikisha ndani ya siku hizo mia moja maeneo hayo yanakuwa wazi.

 

----------------------------MWISHO--------------------------------------

 
 

 

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akioneshwa mchoro wa eneo la wazi katika mtaa wa Surungai eneo la Meriwa kata ya Ipagala jijini Dodoma alopofanya ziara ya kukagua uvamizi wa eneo hilo tarehe 8 Septemba 2023.


Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akioneshwa ramani ya mchoro ya eneo la wazi kwenye mtaa wa Surungai eneo la Meriwa kata ya Ipagala mkoani Dodoma wakati wa ziara ya kukagua uvamizi wa eneo la wazi tarehe 8 Septemba 2023.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa akiwa kwenye ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Ipagala jijini Dodoma alipofanya ziara ya kukagua uvamizi wa eneo la wazi katika mtaa wa Surungai eneo la  Meriwa tarehe 8 Septemba 2023. Wa pili kulia ni Kamishna wa Ardhi Nathaniel Methew Nhonge

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Jerry Silaa (kushoto) akisisitiza jambo kwa mmoja wa wananchi waliouziwa eneo la wazi katika mtaa wa Surungai eneo la Meriwa kata ya Ipagala Bi. Penina Likwelile wakati alipokwenda kukagua uvamizi wa eneo la wazi mkoani Dodoma tarehe 8 Septemba 2023. Kulia ni Mwenyekiti wa Mtaa wa Surungai kata ya Ipagala Gervas Lugunyale.
(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI) 

 

 



 






Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link