Home » » MBUNGE TEMEKE AWEZESHA WANANCHI 3000 KUPATA HUDUMA ZA NIDA NA RITA.

MBUNGE TEMEKE AWEZESHA WANANCHI 3000 KUPATA HUDUMA ZA NIDA NA RITA.

Written By CCMdijitali on Thursday, October 5, 2023 | October 05, 2023




Na:Shalua Mpanda-TMC

Mbunge wa Jimbo la Temeke Mheshimiwa Dorothy Kilave amewezesha Wananchi zaidi ya 3000 kupata huduma ya namba ya utambulisho ya uraia(NIDA)  na huduma ya usajili wa vizazi na Vifo(RITA) katika kata zote 13 za Jimbo hilo.

Akizungumza wakati wa zoezi hilo katika kata ya Yombo Vituka leo Oktoba 5,2023,Mhe Kilave amesema aliona changamoto wanazozipata Wananchi wakati wa upatikanaji wa vitambulisho vya uraia na hati hizo, ndipo akaamua kuanzisha kampeni hiyo kuwasaidia.

"Baada ya kuona changamoto hii niliamua kutafuta vijana ambao nimewawezesha na kupata mafunzo  kutoka NIDA na hapa kinachofanyika ni kuwasaidia Wananchi hawa bure kabisa". Alisema Mbunge huyo


Aidha Mhe.Kilave amesema gharama zote za kujaziwa taarifa kwenye mfumo,kutoa nakala(photocopy),kupiga picha na taratibu nyingine wananchi hao wanazipata bila malipo na gharama pekee ni ile ambayo mwananchi ataenda kulipa kupata kitambulisho baada ya kupewa namba ya malipo(Control number).

Kwa upande wake diwani wa kata ya Yombo Vituka Mhe.Fulgence Lwiza amemshukuru Mbunge huyo na kumuomba aendelee kutoa msaada wa huduma nyingine muhimu zinazowagusa Wananchi moja kwa moja.

Bi.Amina Sultani mkazi wa Yombo Vituka amesema zoezi hilo limewasaidia kupata namba za utambulisho wa uraia kwa urahisi tofauti na kuzifuatilia katika ofisi za Wilaya ambazo amedai kuna usumbufu wa kuzipata.

Zoezi hili limeonekana 'mkombozi' kwa wakazi wengi katika kata zote 13 ambapo wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kupata huduma hii bure iliyoanzishwa na Mbunge huyo kuwasaidia wananchi ambao wengi wao hawana uwezo wa kufanya taratibu zote wao wenyewe bila msaada.











Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link