Kumalizika kwa Barabara ya Handeni hadi kilindi kutawarahishia Wakazi wa Wilaya ya Kilindi na maeneo jirani kutumia kwa usafiri na usafirishaji mazao na kuweza kuongeza kipato cha Mtu mmoja mmoja na Pato la Taifa.
Mlezi wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Tanga Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameyasema hayo akiwa katika muendelezo wa ziara yake ya kuimarisha Chama Wilaya ya Kilindi na Wilaya Handeni.
Amesema kasi ya mradi huo si ya kuridhisha hivyo, ameahidi kuwa Serikali itakaa na mkandarasi kujua changamoto zilizopo ili mradi huo uendelee na kumalizika na hatimae Wananchi waendelee kunufaika na barabara hiyo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inatambua umuhimu wa mawasiliano hasa barabara hivyo, amewataka Wananchi kuwa wavumilivu wakati Serikali ikiendelea kutafuta njia ya kukamilisha barabara hiyo.
Mhe. Hemed ambae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Wananchi wa Kilindi kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia mgogoro wa mpaka baina ya Kiteto na Kilindi na kuwahakikishia kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa maelekezo juu ya kutatua Mgogoro huo na kuwaahidi Wananchi hao kuwa Serikali yao itaumaliza kwa haraka mgogoro huo.
Akizungumzia uimarishaji wa Chama Mhe. Hemed amesema ni wajibu kila Mwanachama wa CCM kufuata Sheria, Kanuni na Miongozo ya Chama na kuwaasa wote wanaopita kutangaza Nia ya kugombea nafasi kabla ya wakati kuacha tabia hiyo na kuiahidi Kamati ya Siasa za Wilaya na Mkoa kuwachukulia hatua stahiki wote wenye tabia hizo.
Aidha amesema ni jukumu la kila Mwanachama wa Chama Cha Mapinduzi kueleza mazuri yanayofanywa na Serikali ili kuzidisha Imani ya wananchi kwa Serikali yao jambo ambalo litasaidia kukipatia ushindi Chama Cha Mapinduzi katika Chaguzi zote zijazo.
Nae Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Waziri Kindamba amesema Serikali ya Mkoa wa Tanga itahakikisha amani na utulivu inaendelea kuwepo Mkoani humo na wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kila siku za kijamii ili kujikimu kimaisha.
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameelekeza kujengwa kwa Skuli ya Sekondari ya Wanawake ambayo itamaliza changamoto ya Wanafunzi kufuata elimu maeneo ya mbali na kumuhakikisha Mlezi huyo kuwa Serikali ya Mkoa wa Tanga itasimamia ujenzi huo kukamilika kwa wakati uliopangwa na kwa ubora ili kuweza kudumu kwa muda mrefu.
Nae Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kilindi Bwana Muhamed Kumbi amemshukuru Mlezi wa CCM Mkoa wa Tanga kwa kuamua kufanya ziara kuonana na Viongozi na Wanachama wa CCM Wilaya zote za Mkoa huo jambo ambalo linaonesha ukomavu wa Chama Cha Mapinduzi kwa kuwajali wanachama wao.
Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeelekeza miradi mingi kwa Wananchi wa Wilaya ya Kilindi inayowagusa Wananchi wa Wilaya hiyo na maeneo jirani ikiwemo Maji, Elimu, na ujenzi wa Barabara unaoendelea.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
10/10/2023
Home »
KITAIFA
,
MIKOANI
» "NI JUKUMU LA KILA MWANACHAMA WA CCM KUELEZA MAZURI YANAYOFANYWA NA SERIKALI" MHE HEMED







