Zanzibar,
27 Oktoba, 2023
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameishukuru Benki ya dunia kwa jitidaha zake za kuendelea kuziunga mkono nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.
Rais Dk. Mwinyi ametoa shukurani hizo, Ikulu, Zanznibar alipozungumza na Mwakilishi Mkazi wa benki hiyo, Nathan Balete na ujumbe wake.
Dk. Mwinyi alimueleza mgeni wake huyo juu ya Zanzibar inavyonufaika na fursa na misaada na mikopo ya gharama nafuu kutoka kwa benki hiyo kupitia mirandi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo zikiwemo sekta za afya, elimu, miundombinu, uchumi wa buluu, uwezeshaji wa Wanawake na mahakama.
Alisema, Zanzibar imekua na miradi mingi ya maendeleo inayoungwa mkono na benki ya dunia kupitia ushirikiano mzuri uliopo baina ya benki hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais Dk. Mwinyi alieleza fursa nyingine ambapo Zanzibar inanufaika kutoka Benki ya dunia ni pamoja na kuwajengea uwezo Wanzania kupitia mikutano ya kimataifa, warsha, makongamano pamoja na misaada ya kiufundi.
Akizungumzia sekta ya nishati hususani umeme wa jua, upepo na suala la gesi asilia, Rais Dk. Mwinyi aliieleza Benki ya dunia kuangalia namna bora ya kuiungamkono Zanzibar kujitegemea kwenye suala zima la kuzalisha umeme wake mwenyewe ili kuwafikishia huduma bora wananchi wake kupitia vyanzo mbalimbali ikiwemo gesi asilia na hewa ukaa.
Dk. Mwinyi alisema, ni jambo la faraja endapo Zanzibar ikipata kujitegemea kuzalisha nishati ya umeme, kwani kwa miaka mingi imekua ikitegemea umeme kutoka Tanzania bara, hivyo alimueleza mgeni huyo nia ya Zanzibar kujitegemee kupata umeme wake.
Pia, Rais Dk. Mwinyi alisifu wazo la Benki ya dunia kuanzisha ofisi zake Zanzibar, litaimarisha uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo baina ya pande mbili hizo mbali na kuungamkono sekta za maendeleo Tanzania ikiwemo Zanzibar.
Naye, Mwakilishi huyo Mkazi wa benki ya dunia Tanzania, Nathan Balete alisifu juhudi za Rais Dk. Mwinyi kwa kuimarisha maendeleo na huboresha huduma bora za jamii kwa wananchi wake ambazo zimeijengea sifa Zanzibar kimataifa.
Nathan Balete, pia anaziwakilisha nchi nyengine tatu za Afrika mbali na Tanzania zikiwemo Malawi, Zambia na Zimbawe, alimweleza Rais Dk. Mwinyi nia ya benki hiyo kutembelea miradi mbalimbali ya maendeleo wanayoiungwa mkono pamoja na wazo lao la kufungua ofisi zao hapa Zanzibar.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Dk. Saada Mkuya Salum alieleza, Zanzibar inatajia kupata heshima kubwa ya kimataifa kwa kutembelewa na viongozi wakubwa duniani akiwemo Rais wa Benki ya dunia, Ajay Singh Banga anaetarajiwa kuhudhuria mkutano wa 20 wa Mapitio ya benki hiyo, unaotoa misaada ya kiufundi na maendeleo kwa miaka mitatu mitatu kwa mataifa yanayoendelea duniani.
Alisema, mkutano huo pia utahudhuriwa na mawaziri wengine akiwemo wazairi wa masuala ya Afrika kutoka Uingereza.
Dk. Mkuya aliitaja Zanzibar kwa mara ya kwanza itakuwa mwenyeji wa Mkutano mkubwa duniani utakaohudhuriwa na wageni mashuhuri mwezi Disemba mwaka huu ambao unaotarajiwa kuhudhuriwa kati ya wageni 300 hadi 350 wenye lengo la kufanya mapitio ya miadi inayoungwa mkono na benki ya dunia pia kuangalia namna bora ya utekelezwaji wa miradi hiyo na namna ya kuongezwa fedha na ruzuku kwa miradi itakayofanya vizuri zaidi na mataifa wanufaika.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi |
IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR.