Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K. Mongella |
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John V.K. Mongella amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri zote za mkoa wa Arusha kuhakikisha vituo vyote vya kutolea huduma za Afya vinafungwa mfumo wa kumeneji taarifa na kukusanyia Mapato wa GoT HoMIS, mfumo ambao licha ya kuthibiti ukusanyaji wa Mapato unasaidia kutunza kumbukumbu za matibabu ya wagonjwa, wanaofika kituoni kuapta huduma za afya.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa agizo hilo wakati akikagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Karatu na kujionea namna mfumo huo wa GoT HoMIS unavyofanya kazi na kusisitiza kuwa kila kituo cha Afya kinalazimika kufungwa na kutumia mfumo huo kama yalivyo maagizo na maelekezo ya Serikali.
Amesema kuwa Serikali imeandaa mfumo huo muhimu kwa lengo la kumeneji huduma zinazotolewa na hospitali kwa wagonjwa pamoja na kudhibiti mianya ya upotevu wa mapato na dawa zinazoingia na kutolewa kwa wagonjwa.
Ameweka wazi kuwa licha ya mahitaji mengi ya Halmashauri, Halmashauri zinatakiwa kuweka kipaumbele kwenye bajeti zao kwa ajili ya kufunga mifumo hiyo ili kuboresha utoaji na upatikanaji wa huduma za afya zenye ubora kwa wananchi ambalo ndilo lengo kuu la Serikali ya awamu ya sita la kujenga vituo hivyo karibu na maeneo ya wananchi.
"Kupitia mfumo huo tutapata takwimu sahihi za wagonjwa, wanaohudumiwa kwa siku, matibabu waliyopatiwa, dawa walizotumia pamoja na kiasi cha fedha kilichokusanywa, Mfumo huu ni muhimu sana licha ya kuwa wapo wahudumu wasiopenda kuutumia, ifike mahali tuhame kwenye mifumo ya analojia tuingie kwenye utoaji huduma wa Kidigitali kwa kuwa unaokoa muda pia" Ameweka wazi Mhe. Mongella
Awali Mkuu huyo wa Mkoa ametembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi wa Hospitali hiyo ya wilaya mradi unatekelezwa na Serikali kwa gharama ya zaidi ya Bilioni 3.5 lengo likiwa ni kusogeza utoaji na upatikanaji wa huduma za afya karibu na wanachi
Ikumbukwe kuwa, ujenzi wa Hospitali za wilaya ni Utekelzaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM, Ibara ya 81 Ujenzi na Ukarabati wa Vituo vya Kutolea Huduma ya Afya ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Hospitali za Wilaya nchini
#ArushaFursaLukuki