Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb.) amesaini kitabu cha maombolezo Ubalozi wa Finland kufuatia kifo cha Rais wa zamani wa nchi hiyo Mhe. Martti Ahtisaari kilichotokea tarehe 16 Oktoba 2023.
Mhe. Ahtisaari amefariki akiwa na umri wa miaka 86, alikuwa Rais wa Finland kuanzia mwaka 1994 hadi 2000 na Balozi Mstaafu wa Finland nchini Tanzania mwaka 1973 hadi 1976
Mara baada ya kusaini kitabu cha maombolezo, Balozi Mbarouk amesema Hayati Ahtisaari atakumbukwa daima kama mwanadiplomasia mashuhuri ambaye alijitolea maisha yake yote katika masuala ya upatanishi
“Kiongozi huyo atakumbukwa kama kiongozi mahiri wa Finland aliyeimarisha ushirikiano wa karibu Kati ya Finland na Tanzania kupitia cheo chake cha Ubalozi alichohudumu nchini mwaka 1973-1976 .
Kupitia nyadhifa hiyo Hayati Ahtisaari alifanya kazi kama rafiki wa karibu na Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Hayati Benjamin William Mkapa na Mhe. Dkt. Jakaya Kikwete.
Kupitia urafiki huo, Hayati Ahtisaari alishirikiana na MaRais Wastaafu kuanzisha mikakati ya kutafuta amani kwenye nchi zenye migogoro barani Afrika hususan Burundi kupitia Taasisi ya Mpango wa Utatuzi wa Migogoro (CMI) ambaye ndiye mwanzilishi.
Kwa kutambuliwa kama mpatanishi wa amani, Hayati Ahtisaari alitunukiwa medani ya amani duniani ya Nobel mwaka 2008 na alisifiwa kwa kukuza undugu baina ya Mataifa kwa mtindo wake wa kujitolea bila kujionesha
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tunapenda kutoa salamu zetu za pole kwa wananchi na serikali ya Finland pamoja na familia kwa kuondokewa na kiongozi bora na mpenda amani. Mungu ampumzishe kwa amani,” aliongeza Mhe. Balozi Mbarouk
@wizara_mambo_ya_nje_tz