Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani zimeeleza dhamira yao ya kujikita zaidi katika kuendeleza na kukuza ushirikiano wa kijamii na kiuchumi kwa maendeleo ya pande zote mbili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan (Julia) na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier (kushoto) |
Hayo yamebainishwa na Viongozi Wakuu wa mataifa hayo mawili rafiki, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ikulu, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo Rais Samia ameeleza kuwa licha ya Tanzania na Ujerumani kuwa ushirikiano mzuri na wa muda mrefu katika shughuli mbalimbali za maendeleo hususani katika sekta ya Afya, elimu, usambazaji wa maji safi na salama, hifadhi ya mazingira, ulinzi na usalama, haki za binadamu na utawala bora na hifadhi ya maliasili bado kuna fursa kubwa ya kukuza zaidi ushirikiano wa kibiashara na uchumi kwa manufaa ya watu wa pande zote mbili.
“Katika mazungumzo yetu tumeelekeza timu za pande zote mbili kukaa na kufanya majadiliano ya mara kwa mara ili kubaini maeneo mapya ya ushirikiano ambayo yatatusaidia kupiga hatua kwa haraka zaidi katika kukuza biashara na uwekezaji kwa manufaa ya watu wetu” Alisema Rais Samia.
Katika hatua nyingine Rais Samia ameeleza kuwa katika mazungumzo na mgeni wake Rais Frank-Walter Steinmeier wamekubaliana kufungua majadiliano katika masuala kadhaa ya kihistoria ikiwemo kuhusu suala la mabaki ya kale ya Tanzania yaliyohifadhiwa nchini Ujerumani.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani Mheshimiwa Frank-Walter Steinmeier ameeleza kuwa Ujerumani itaendelea kufungua milango ya ushirikiano zaidi kwa Tanzania katika kijamii na kiuchumi kwa maendeleo ya sasa na vizazi vijavyo.
“Ujerumani tutatendelea kujikita katika kuangazia maeneo mapya ya ushirikiano ikiwemo kuongeza nguvu ya kusaidia maendeleo ya nishati jadilifu nchini Tanzania na uchumi wa kidijiti ambao utatengeneza ajira nyingi zaidi kwa vijana. Tunafanya haya yote tukiamini kuwa hatusherekei urafiki wetu pekee bali maendeleo ya kiuchumi” Alieleza Rais Frank-Walter Steinmeier
Mbali masuala ya biashara na uchumi Rais Frank-Walter Steinmeier ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita ikiongozwa na Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa hatua kubwa iliyopiga katika kuboresha mazingira ya Demokrasia, Haki za Binadamu na Utawala Bora.
Rais Frank-Walter Steinmeier ametumia fursa hiyo kuzishukuru familia za wahanga wa Vita vya Majimaji za jijini Songea kwa kumwalika kuzitembelea huku akieleza kuwa ni faraja kubwa kwake ikiwa ni mwendelezo wa ishara ya utayari wa kusonga mbele pamoja licha ya yaliyojiri katika historia.