MHE.MCHENGERWA: WATUMISHI WA AFYA 10,305 KUAJIRIWA MWAKA WA FEDHA 2023/24
OR-TAMISEMI
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Mohamed Mchengerwa amemshukuru Rais Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kukubali ombi la kuajiri watumishi wengine wa afya 10,305 kwa mwaka wa fedha 2023/24 ambao watapangwa kwenye Vituo vipya vya kutolea huduma za Afya ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
Akizungumza Oktoba 28, 2023 jijini Dar es salaam kwenye uzinduzi wa ripoti ya Afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya Maralia kwa Mwaka 2022, Mhe.Mchengerwa amesema maboresho ya miundombinu yanayofanyika yanakwenda sambamba na upatikanaji wa rasilimali watu ambapo OR-TASMISEMI imeajiri watumishi wa kada za Afya 17,950 katika kipindi cha miaka miwili na wengine 10,305 wanatarajiwa kuajiriwa kwa Mwaka wa fedha 2023/24.
“Vituo vya kutolea huduma za Afya vilivyokuwa vimekamilika sasa vinaenda kuanza kutoa huduma kwa wananchi, Aidha, nichukue nafasi hii kuwasisitiza sana Wakuu wa Mikoa na Wilaya kuhakikisha kuwa Vituo vya kutolea huduma za Afya ambavyo vimeishakamilika vinaanza kutoa huduma za Afya kwani watumishi na vifaa tiba kwa kiasi kikubwa vimetolewa.”
“Serikali imejenga miundombinu bora ya Vituo vya kutolea huduma za Afya nchini kwa gharama kubwa na kuweka Vifaa na vifaa tiba, hivyo nawataka watumishi waliopewa dhamana ya kuwahudumia wananchi katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini, kuhakikisha wanatoa huduma bora na kuwa na kauli nzuri kwa wateja,”amesema.
Amesisitiza kuwa atahakikisha anawachukulia hatua za kinidhamu watumishi wote wataokaobainika kuzembea katika kuwahudumia wananchi.
“Natumia fursa hii pia kutoa wito kwa wananchi wanaofuata huduma katika vituo vyetu vya kutolea huduma za afya kutosita kutoa tarifa za watumishi wasio waadilifu, wazembe na wanaoshindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo ili niweze kuchukua hatua stahiki kwa wakati kupitia kituo cha huduma kwa mteja kupitia namba 0735-160210 na 0262 – 160210,” amesema.