Home » » DKT. BITEKO AIAGIZA TPDC KUANDAA MPANGO WA MUDA MREFU WA UPATIKANAJI GESI NCHINI

DKT. BITEKO AIAGIZA TPDC KUANDAA MPANGO WA MUDA MREFU WA UPATIKANAJI GESI NCHINI

Written By CCMdijitali on Tuesday, November 21, 2023 | November 21, 2023


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza Bodi na Menejimenti ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kuja na mpango wa muda mrefu utakaoonesha jinsi nchi itakavyoweza kuongeza kiasi cha gesi asilia

Amesema kuwa kufanya hivyo kutawezesha kuwepo kwa hazina ya kutosha ya nishati hiyo inayotumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kuzalisha umeme, viwandani, majumbani na katika magari.

Dkt. Biteko ameyasema hayo tarehe 21 Novemba, 2023 wakati wa kikao chake na Bodi na Menejimenti ya TPDC ambacho kililenga kufahamiana, kubadilishana mawazo juu ya utendaji kazi na Mhe. Dkt. Doto Biteko kuelekeza matarajio ambayo nchi inayahitaji kutoka TPDC.

“TPDC tujiulize, Je uwezo wetu wa kuzalisha Gesi Asilia unaweza kujibu mahitaji yetu  ya Gesi ? tujiulize hili na tuchukue hatua. Tutambue kuwa mahitaji ya Gesi Asilia ni makubwa kwa sasa kwani dunia inahama kutoka matumizi ya mafuta na kwenda kwenye Gesi Asilia hivyo lazima tujipange, na pia tukumbuke tumesaini makubaliano ya kusafirisha nishati hii kwenda Uganda, Zambia na Kenya hivyo lazima tuwe na Gesi ya kutosha.” Amesisitiza Dkt. Biteko.

Dkt. Biteko pia amewataka TPDC kutokuwa na urasimu katika uchukuaji wa maamuzi mbalimbali ikiwemo kwenye shughuli za utafiti wa Mafuta na Gesi Asilia ili kutorudisha nyuma sekta hiyo nchini.

Kuhusu maelekezo aliyoyatoa wakati wa ziara yake, katika Kisiwa cha Songosongo mkoani Lindi na Kijiji cha Madimba na Msimbati mkoani Mtwara, Dkt. Biteko amesisitiza kuwa, maisha ya wananchi katika maeneo hayo ambayo kuna visima na mitambo ya Gesi Asilia lazima yabadilike na wapewe huduma bora ikiwemo maji, umeme, afya na usafiri.

“Nashukuru mmeanza kufanyia kazi maagizo niliyoyatoa kwa haraka, ikiwemo ya kuweka taa za barabarani Kijiji cha Msimbati, kupeleka umeme wa uhakika Madimba na Msimbati unaotoka kwenye mitambo ya Gesi Asilia, kupeleka kivuko kisiwa cha Songosongo na malipo ya mafao kwa wastaafu wa Knight Support ambao walikuwa wakilinda mitambo na visima vya Gesi Asilia Songosongo ambao hawakulipwa muda mrefu, watu hawa wanahitaji huduma bora.”


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link