Home » » MHE. BITEKO ATOA MAAGIZO KWA MSAJILI WA HAZINA

MHE. BITEKO ATOA MAAGIZO KWA MSAJILI WA HAZINA

Written By CCMdijitali on Friday, November 17, 2023 | November 17, 2023

MHE. BITEKO ATOA MAAGIZO KWA MSAJILI WA HAZINA KUELEZA SABABU YA MASHIRIKA YA UMMA KUTOSHIRIKI SHIMMUTA 2023


Na Shamimu Nyaki

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Doto Biteko amemuagiza Msajili wa Hazina kufikia Jumatatu Novemba 20, 2023 awasilishe taarifa kwa nini mashirika mengi ya Serikali hayajatoa kibali kwa watumishi wao kushiriki Mashindano ya Taasisi, Mashirika ya Umma na Binafsi (SHIMMUTA) mwaka 2023 jijini Dodoma.

Mhe. Biteko ametoa maagizo hayo wakati akifungua mashindano hayo Novemba 17, 2023 Uwanja wa Jamhuri Dodoma ambapo amebaini mashirika ya umma yapatayo 248 nchini hayakushiriki mashindano hayo huku mashirika 54 pekee ndio yametoka kibali kwa watumishi wao kushiriki mashindano hayo.

"Naipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kuendelea kusimamia vyema michezo, kwa sasa tunashuhudia nchi yetu ikitangazwa vyema na hivi karibuni tumepata uwenyeji wa Mashindano ya AFCON mwaka 2027 kwa kushirikiana na wenzetu wa Kenya na Uganda" Mhe. Doto Biteko.

Mhe. Biteko amewaasa wanamichezo hao kutumia michezo hiyo kubadilishana uzoefu, kupeana mbinu za mafanikio lakini pia kujifunza kuweka alama mahali wanapofanyia kazi pamoja na kutimiza wajibu wa kuhakikisha wanatatua matatizo ya wananchi kupitia sehemu za kazi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma amezipongeza Taasisi za Serikali, Mashirika ya Umma na Binafsi yaliyotoa ruhusa kwa Watumishi kushiriki mashindano hayo, akisema ni hatua nzuri ya kuunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendeleza michezo nchini.


"Katika kipindi hiki cha Serikali ya Awamu ya Sita, tumeshuhusia Maendeleo makubwa katika Sekta ga michezo ikiwemo kupata uwenyeji wa Mashindano ya AFCON mwaka 2027, Klabu ya Simba kucheza hadi robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2022/ 23 na Klabu ya Yanga kucheza hadi Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2022/23" amesema Mhe Mwinjuma.

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Ndg. Gerson Msigwa amesema lengo la Mashindano hayo ni kuimarisha afya za watumishi na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, huku akitoa rai kwa makampuni, taasisi za Serikali na binafsi kutekeleza  maelekezo ya Serikali ya kufanya mazoezi na kushiriki mashindano mara kwa mara.

Mashindano hayo yanajumuisha michezo 12 ikiwemo Mpira wa Miguu, Netiboli, Mpira wa Wavu, Riadha, Kivuta Kamba, na mingine ikihusisha wamichezo 3478.








Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link