Zanzibar,
06 Disemba, 2023
SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema imeweka kipaumbele kwenye kukuza uchumi wake na kuongeza uwekezaji wa huduma za jamii ikiwemo afya, elimu, afya na huduma nyingine za jamii ikiwemo kuimarisha umeme na maji safi vijijini.
Aidha, imeeleza inavyojikita kwenye kilimo kinachozingatia zaidi hali ya hewa ili kuendana sambamba na nyakati za mavuno kwa lengo la kuwaletea tija Watanzania.
Akizungumza kwenye ufunguzi wa mkutanao wa Kimataifa wa tathmini ya muda, kati ya mzunguko wa 20 wa Mapitio ya benki ya Dunia (IDA) kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ukumbi wa Golden Tulip, Uwanja wa ndege, Zanzibar, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema, Tanzania inavyoshirikiana na Benki ya Dunia kwa kufanyakazi madhubuti ya kuwaondoa mamilioni ya watu kutoka kwenye umaskini na kuwaletea mabadiliko kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na benki hiyo.
Alisema, Tanzania imezindua mpango wa “Kujenga Kesho Bora” ambapo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaidia wanawake na vijana wengi kupatiwa mafunzo, rasilimali ardhi kwa ajili ya kilimo cha kisasa, kuwawezesha kiuchumi, pembejeo na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo na ufugaji katika kujitegemea wenyewe kiuchumi na kujikimu.
“Tunashukuru Benki ya Dunia na washirika wengine kwa msaada wao kwa mpango huu”. Alishukuru Dk. Samia.
Rais Dk. Mwinyi alieleza, kwa msaada wa IDA wa dola za Marekani milioni 200 kwa Mpango wa Umeme Vijijini umeisaidia Tanzania kuwafikia zaidi ya watu milioni 2.5, hali iliyoisaidia nchi kufikia viwango vya upanuzi wa haraka barani Afrika kwa kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Alisema, zaidi ya watu milioni 4.5, wamefikiwa na huduma bora za jamii ikiwemo umeme vijijini, hospitali na ujenzi wa shule za vijijini.
Alisema mpango huo uliongeza fursa za ajira, biashara na matokeo bora kwa wanafunzi walioishi maeneo mbali na shule. Pia alisema, mpango ulikuwa na matokeo mazuri kiasi ya kuvutia ufadhili wa ziada wa dola za Marekani milioni 335 kusaidia kufikia matokeo bora zaidi kwa jamii za vijijini.
Akizungumzia sekta ya maji, chini ya miaka mitano ya mfuko wa msaada wa dola za Marekani milioni 300 kwa ajili ya Mpango Endelevu wa Ugavi wa Maji Vijijini na Usafi wa Mazingira uliwezesha upatikanaji wa maji safi kwa zaidi ya watu milioni 4.7, nusu yao wakiwa wanawake.
Alieleza, mpango huo pia uliboresha upatikanaji wa huduma za vyoo kwa zaidi ya watu milioni 6.6, vituo vya afya 1,904 na skuli za msingi 1,095.
Pia, Rais Dk. Mwinyi alizungumzia mkutano wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya Tabianchi (COP28) uliofanyika Dubai ambako Rais Dk. Samia alitetea ajenda ya kusaidia kupunguza nishati mimea zinazoathiri mazingira mara baada ya kuongoza uzinduzi wa mradiri wa nishati safi ya kupikia itakayowanufaisha wanawake wengi, Afrika (AWCCSP).
Akizungumzia Zanzibar inavyonufaika na fursa kutoka Benki ya Dunia, Rais Dk. Mwinyi alieleza uchumi wa Zanzibar unategemea Utalii kwa kiasi kikubwa hasa utalii wa utamaduni. Alisema, hifadhi ya Mji Mkongwe ambao ni urithi wa Dunia wa UNESCO, ulinufaika na Benki ya Dunia kupitia mradi wa “huduma za Mijini, Zanzibar” (ZUSP) ambao ulipata msaada kutoka IDA wenye thamani ya dola za Marekani milioni 93 ili kuboresha upatikanaji wa huduma za mijini na kuhifadhi urithi huo wa kitamaduni.
Alieleza pia mradi huo ulikarabati kipande cha mita 340 cha ukuta wa bahari ya Mizingani uliokuwa hatarini kuporomoka na kuzorotesha usafiri wa kivuko kwa wafanyabiashara na watalii. Sambamba na kuboresha barabara kuu ya Mji Mkongwe.
Alieleza Benki ya Dunia pia imesaidia Tanzania kupitia Mitandao ya Hifadhi ya Jamii ambayo ilitolewa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na Mradi wa Ushirikiano wa Usafiri kwa ajili ya kuboresha barabara.
Alisema, ushirikiano mwema uliopo baina ya Tanzania na Benki ya Dunia umesaidia maisha ya mamilioni ya watu nchini nakuongeza kuwa ushirikiano huo utaendelea kudumu.
Rais, Dk. Mwinyi aliiomba Benki ya Dunia na washirika wake, kuendelea kuimarisha usaidizi wao kwa nchi wanufaika wa IDA ili kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs).
Pia Dk. Mwinyi aligusia eneo la biashara huria kwa mataifa wanufaika wa Benki ya Dunia na washirika wake, ili kuimarisha ushindani na uundaji wa nafasi za kazi kupitia ushirikiano wa kikanda na biashara, kwa bara la Afika na maeneo mengine ya dunia,
“Tunaamini IDA na IFC zinahitaji kuongeza usaidizi ili kukuza sekta binafsi inayostawi, jambo la msingi ni kuunganisha biashara za Kiafrika katika minyororo ya thamani ya kimataifa na kuvutia FDIs.” Alieleza Rais Dk. Mwinyi.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Rais wa Benki ya Dunia na washirika wake, Ajei Banga alimpa pole Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan kwa mtihani wa majanga ya kimaumbile yaliyowakumba Watanzania wa Manyara, nakueleza kuwa Benki ya Dunia ilipokea taarifa kwa masikitiko makubwa.
Mapema akizungumza kwenye mkutano huo waziri wa Fedha wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Lameck Nchemba aliiomba Benki ya Dunia kuwaongeza watanzania wa Mkoa wa Manyara walioathiriwa na mafuriko hivi karibuni kupitia fao la benki hiyo la majanga ya kimaumbile.
Naye, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Dk. Saada Mkuya Salum, alieleza mafanikio makubwa ya mkutano huo wa Kimataifa wa tathmini ya muda, kati ya mzunguko wa 20 wa Mapitio ya benki ya Dunia (IDA) yamefikiwa kutokana na jukudi kubwa za uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa ushirikiano wa karibu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na msaada mkubwa waliopata kutoka kwa Mwakilishi Mkaazi wa benki hiyo, Bw. Nathan Balete.
Zaidi ya wageni 300 kutoka mataifa mbalimbali dunia wamehudhuria mkutano huo wenye lengo la kufanya mapitio ya miradi inayoungwa mkono na benki hiyo, pamoja na mambo mengine pia utaangalia namna bora ya utekelezwaji wa miradi ya maendeleo na namna ya kuongezwa fedha na ruzuku kwa miradi itakayofanya vizuri zaidi kwa mataifa wanufaika.
IDARA YA MAWASILIANO IKULU, ZANZIBAR.