Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuimarisha huduma za kijamii zikiwemo Afya, Elimu na Maji safi na salama.
Ameyasama hayo alipokuwa akiuakhirisha Mkutano wa Kumi na Tatu(13) wa Baraza la Kumi (10) la Wawakilishi katika Ukumbi wa Baraza la Wawakilishi Chukwani Jijini Zanzibar.
Mhe. Hemed amesema Serikali itaendelea kusimamia Miradi ya Ujenzi wa Skuli, Hospitali na Miradi ya Maji safi na salama kwa lengo la kuhakikisha Wananchi wanapata huduma hizo katika maeneo ya karibu ikiwa ni utekelezajiwa Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020-2025 pamoja na ahadi zilizotolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe Dkt Hussen Ali Mwinyi wakati wa Kampeni za Uchaguzi 2020.
Amesema kuwa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar ipo katika hatua za kuboresha Daftari la wapiga kura ambapo amewahimiza Wananchi kuitumia nafasi yao ya kidemokrasia kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kufata maelekezo yanayotolewa na Tume ya Uchaguzi.
Aidha Mhe. Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali itahakikisha inapambana kwa nguvu zake zote kuondosha kabisa vitendo vya utumiaji wa dawa za kulevya na vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia wa wanawake na watoto ambavyo vinaendelea kuiathiri Jamii ya Wazanzibari.
Sambamba na hayo amesema katika kuhakikisha mapato ya Serikali yanazibitiwa, Serikali imeimarisha Mfumo wa usimamizi wa fedha wa IFMIS na kuanzisha Mfumo wa Zan-malipo, mfumo wa manunuzi wa E- Proz, mfumo wa ukusanyaji wa kodi wa kutumia mashine ya( EFD) mfumo wa payroll na mfumo wa bajeti na matumizi (BAMAS).
Amefahamisha kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea kuchukua jitihada mbali mbali katika kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuboresha maslahi ya wafanyakazi, hivyo amewataka watumishi kuendelea kuimarisha nidhamu na uwajibakaji kwa maslahi mapana ya nchi.
Mhe. Hemed amesema kuwa michezo ni jambo muhimu linalowaunganisha wananchi walio wengi Duniani hivyo Serikali inakamilisha ukarabati wa Ujenzi wa Kiwanja cha Amani Unguja na Gombani Pemba ambapo kukamilika kwake mandhari na haiba ya viwanja hivyo yatakuwa na muonekano wenye hadhi ya Kimataifa.
Sambmba na hayo Mhe. Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameipongeza Timu ya Vijana chini ya Umri wa miaka 15 Karume Boys kwa kutwaa Ubingwa wa mashindano ya CECAFA 2025 yaliyofanyika Uganda na kupata Mkono wa Dhahabu wa Kipa bora jambo ambalo limeiletea heshima nchi yetu.
Mhe. Hemed ametoa pole kwa wananchi walioatirika na Mafuriko ndani ya Zanzibar na Tanzania Bara hasa kwa wakazi wa Manyara kufuatia Mafuriko ya Maporomoko ya Udongo yaliyotokea katika Kijiji cha Katesh na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 68 na majeruhi zaidi ya 100.
Katika Mkutano wa Kumi na Tatu(13) wa Baraza la Kumi(10) la Wawakilishi, Baraza limepokea, limejadili na kupitisha Miswaada Sita(6) ya Sheria pamoja na kuwasilishwa Barazani Ripoti ya Saba ya Utekelezaji wa Tume ya Maadili kwa mwaka 2022/2023.
Imetolewa na kitengo cha Habari (OMPR)
Leo tarehe 08.12.2023