Wazanzibari na Waumini wa Dini ya Kiislamu wametakiwa kuwalea watoto wao kwa kuzingatia Mila, Silka na Desturi za kizanzibari ili kupata kizazi chema chenye Kufuata maadili.
Hayo yamesemwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla wakati akiwasalimia waumini wa Masjid Maungani mara baada ya kumaliza Ibada ya Sala ya Ijumaa.
Amesema wazazi na walezi wanapaswa kuwalea watoto wao kwa kufuata silka na mila za kizanzibari jambo ambalo kitasaidia kuondosha kabisa vitendo vya udhalilishaji hasa kwa wanawake na watoto jambo ambalo linaiharibu sifa Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema ni wajibu wa kila Mzanzibari kupiga vita suala la udhalilishaji na kuwataka wakaazi wa Maungani na maeneo jirani kuhakikisha wanapita nyumba hadi nyumba kupiga vita vitendo vya udhalilishaji na kuhakikisha wanawafichua wale wote ambao wanatabia ya kufanya vitendo hivyo,.
Alhajj Hemed amewataka waumini na Wazanzibari kushirikiana na kuacha muhali na kwenda kutoa ushahidi Mahakamani pale ambapo wanatakiwa kufanya hivyo ili waweze kuchukuliwa hatua kali za kisheria.
Akizunguzia suala la madawa ya kulevya Alhajj Hemed amewataka wananchi wa Zanzibar kuachana na tabia ya kuwakodisha nyumba watu ambao hawawafahamu na hawana taarifa zao za kutosha ili kuondosha wimbi la watumiaji na wauzajiwa wa madawa ya kulevya nchini.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amesema Serikali ya Awamu ya Nane inayoongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt. Hussein Ali Mwinyi itahakikisha inaondosha kabisa suala la madawa ya kulevya kwa kuweka sheria ngumu amabzo zitawabana waingizaji, wasambazaji na watumiaji wa madawa ya kulevya.
Akitoa Khutba katika Sala ya Ijumaa, Maalim SULEIMAN MWINCHUMU amewataka waumini wa Dini ya Kiislam kuchunga nafsi zao na kujielekeza katika kufanya amali njema ambazo zitawaepusha na kupata hasara hapa duniani na kesho akhera.
Amesema kuwa wazazi watakapo weza kuchunga nafsi zao pamoja na kuwachunga watoto dhidi ya wao katika kujiunga na vikundi viovyo watakuwa wameisaidia jamii na taifa kwa ujumla kwaani Taifa lenye maendeleo linahitaji nguvu kazi isiyo na mmong’onyoko wa maadili.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
Leo tarehe..08.12.2023