NA MWANDISHI WETU,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, amesema Wajumbe wa Sekretarieti ya Kamati Maalum ya NEC CCM Taifa Zanzibar wamepitisha pendekezo la kuishauri Kamati Maalum ya NEC kuridhia kuongeza muda wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi kuongoza nchi katika muhula wake wa kwanza kwa kipindi cha miaka saba badala ya mitano.
Hayo ameyaeleza wakati akifunga Mkutano wa Baraza Kuu la UVCCM Wilaya Dimami kichama Zanzibar uliofanyika katika Ofisi za Wilaya hiyo Kiembesamaki.
Dkt.Dimwa,alieleza kuwa maamuzi hayo ya kumuongezea muda wa kuongoza nchi Dk.Mwinyi yanatokana na kuridhishwa na kasi yake ya kiutendaji katika kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 kwa zaidi ya asilimia 100 ndani ya kipindi miaka mitatu na miezi kadhaa toka aingie madarakani.
Katika maelezo yake Naibu Katibu Mkuu huyo Dkt.Dimwa, alieleza kuwa CCM Zanzibar imeona Serikali kuingia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 ni hasara na matumizi mabaya ya fedha za walipa kodi kwani wananchi wanahitaji maendeleo endelevu hivyo Rais Dk.Mwinyi anafaa kuongezewa muda ili Zanzibar iwe nchi ya visiwa iliyoendelea kiuchumi katika ukanda wa Afrika mashariki.
" Wajumbe wa Sektetarieti tumejadili na kutathimini kwa kina juu ya utendaji wa Rais Dk.Mwinyi, tukajiridhisha kuwa hakuna mbadala wake na anastahiki aongoze nchi kwa kipindi cha miaka saba ili apate muda mzuri wa kufanya Mapinduzi ya kimaendeleo katika nyanja za kiuchumi na kijamii.
Maamuzi yetu yatafuata taratibu za kikatiba na kikanuni kwa kuyawasilisha katika vikao vya ngazi za juu ili vitoe baraka zake ili hoja hii ikapitishwe katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar ili yaendelee kufanyika mabadiliko ya baadhi ya vipengele vya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kwa lengo kuhakikisha tunafanya Uchaguzi Mkuu wa dola kwa kila baada ya miaka saba.", alifafanua Dkt.Dimwa.
Alieleza kuwa Wanachama wa CCM na Wananchi kwa ujumla visiwa vya Zanzibar wanampenda,kumthamini na kuridhishwa na utendaji wa Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi kwani amekuwa kiongozi bora katika kutatua kero za wananchi kupitia uimarisha wa sekta mbali mbali za umma na binafsi.
Pamoja na hayo Naibu huyo alisema kila mwananchi mwenye uzalendo na utimamu wa akili anajua maendeleo yaliyotekelezwa visiwani Zanzibar katika sekta ya afya,elimu,usafiri wa anga na majini,uwekezaji,barabara za kisasa,uwezeshaji wananchi kiuchumi,utalii,michezo na miundombinu bora ya biashara na ujasirimali.
Kupitia kikao hicho Dkt.Dimwa, alifafanua juu ya hoja ya ACT-Wazalendo kudai kuwa nchi ina deni kubwa ambapo alieleza kuwa suala la mikopo kwa ajili ya uimarishaji maendeleo ya nchi sio dhambi au uvunjaji wa sheria za nchi kwani hakuna nchi yoyote duniani inayojiendesha kiuchumi kwa fedha zake za ndani bila kukopa benki ya Dunia au nchi zilizoendelea kiuchumi.
Alisema CCM inafanya siasa za kisayansi kwa kusimamia utekelezaji wa sera na mikakati yake kwa vitendo vinavyoonekana na sio porojo na ahadi hewa.
MWISHO