Home » » WAZIRI MAKAMBA AONGOZA KIKAO CHA MAWAZIRI 15 WA EAC

WAZIRI MAKAMBA AONGOZA KIKAO CHA MAWAZIRI 15 WA EAC

Written By CCMdijitali on Saturday, July 6, 2024 | July 06, 2024




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb) akiongoza Mkutano wa faragha wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika Zanzibar. Kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri la EAC Mhe. Deng Alor Kuol wa Sudan Kusini na kulia ni Bi. Veronica Nduva Katibu Mkuu EAC wakati wa ufunguzi wa mkutano huo




Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. January Makamba (Mb) ameongoza Mkutano wa faragha wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika Zanzibar. 

Akizungumza katika Mkutano huo wa siku tatu ambao yeye ni mwenyekiti, Mhe. Makamba amesema Tanzania imejidhatiti kuhakikisha Jumuiya ya Afrika Mashariki inakuwa imara, yenye umoja na inayofikia malengo yake. 

“Madhumuni ya mkutano huu ni kuifanya familia yetu kuwa imara, kuifanya Jumuiya ya Afrika Mashariki kutekeleza majukumu yake vizuri, Tanzania kama moja ya waanzilishi wa Jumuiya hii tumejidhatiti kuona jumuiya ikiwa na umoja, imara na yenye kufanikiwa” alisema Mhe. Makamba 

Naye Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Musalia Mudavadi ameipongeza Tanzania kwa kukubali kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kuongeza kuwa ni wakati muafaka kwa nchi wanachama kuhakikisha wanatumia fursa mbalimbali ndani ya jumuiya kwa manufaa ya wananchi.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Afrika Mashariki wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Rebecca Kadaga ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo na kupongeza juhudi za kuimarisha jumuiya. 

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri Mhe. Deng Alor Kuol amesema kufanyika kwa mara ya kwanza kwa mkutano huo ni jambo jema hasa ikizingatiwa kuwa utaangalia masuala ya amani, usalama na mtangamano wa jumuiya ikiwa ni hatua za kuifanya jumuiya kusonga mbele. 

Mkutano huo wa faragha unajadili taarifa ya Mwenyekiti wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya; hali ya amani, usalama, siasa na uhusiano kati ya nchi wanachama; kutathmini na kujadili mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na masuala yanayokwamisha ufikiwaji wa malengo ya programu na miradi inayopangwa.

Mkutano kazi huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliofanyika kwa njia ya mtandao tarehe 07 Mei, 2024.

Mawaziri kutoka nchi Nane Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki za Burundi, DRC, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Uganda, na Mwenyeji Tanzania wanahudhuria mkutano huo. Mkutano huo pia unahudhuriwa na Makatibu Wakuu kutoka wizara hizo pamoja na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Washiriki wa Mkutano wa faragha wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika Zanzibar katika picha ya pamoja baada ya ufunguzi wa mkutano huo


Washiriki wa Mkutano wa faragha wa Mawaziri wa Mambo ya Nje na Mawaziri wanaoshughulikia masuala ya Afrika Mashariki katika Jumuiya ya Afrika Mashariki unaofanyika Zanzibar wakiimba wimbo wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kabla ya kuanza kikao hicho


Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link