Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amezindua rasmi Ripoti ya Mapitio ya Hali ya Mwenendo wa Uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2024, iliyoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), yenye kauli mbiu isemayo “Driving Tanzania’s Transformation - The Reform of the Global Financial Architecture”.
Mhe. Dkt. Nchemba, amezindua Ripoti hiyo kwa njia ya mtandao akiwa Abuja nchini Nigeria, ambako anaongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mikutano ya Nchi za Afrika (African Caucus Meetings), wanachama wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).
Ripoti hiyo inaonesha kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa kiuchumi na kijamii na kuwa kinara miongoni mwa nchi za Afrika Mashariki, licha ya changamoto zinazoikabili Dunia ikiwemo athari za UVIKO-19, mabadiliko ya tabianchi na mizozo ya vita inayoendelea maeneo mbalimbali duniani.
Dkt. Nchemba amebainisha kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha Uchumi wake kupitia Mpango wake wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP III), wenye lengo la kujenga uchumi imara, shirikishi na wenye ushindani kupitia sekta za uzalishaji, ikiwemo kilimo, uzalishaji viwandani, kuongeza thamani ya bidhaa, uwekezaji na biashara pamoja na kukuza ajira kwa wananchi hususan vijana.
Amezitaka Taasisi za Fedha za Kimataifa, ikiwemo Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), kuweka mazingira ya upatikanaji wa fedha zenye masharti nafuu ili kuziwezesha nchi za Afrika kuwa na uwezo endelevu wa kutekeleza mipango ya maendeleo kwa ajili ya nchi zao.
Dkt. Nchemba alitaja eneo linalokwamisha maendeleo ya nchi hizo za Kiafrika ikiwemo Tanzania kuwa ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi ambapo kila mwaka Tanzania inahitaji dola za Marekani bilioni 6.3 za kukabiliana na hali hiyo zikiwemo athari za papo kwa papo zinazotokana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Ripoti hiyo ya Mwenendo wa Uchumi wa Tanzania iliyowasilishwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika inaonesha kuwa uchumi wa Tanzania umezidi kuimarika na unatarajia kupanda kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023, hadi asilimia 5.7 mwaka 2024, na utafika asilimia 6 mwaka 2025.
Tanzania imesifiwa pia kwa kufanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei na kubaki katika wigo wa chini ya asilimia 3.3 kutokana na sera bora za kiuchumi zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita.
Ripoti hiyo imezitaja sekta zilizochangia ukuaji huo wa uchumi kuwa ni pamoja na sekta ya fedha, huduma, kilimo, kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji, biashara, na sekta ya madini.
Benki ya Maendeleo ya Afrika imeishauri Tanzania kuendelea kusimamia vizuri sera zake za fedha na uchumi, kwa kuendelea kuwekeza zaidi kwenye sekta za uzalishaji, kilimo, nishati na kuboresha zaidi mazingira ya uwekezaji pamoja na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Uzinduzi huo wa Hali ya Uchumi wa Tanzania, umehudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Viongozi waandamizi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, AfDB, Wachambuzi wa masuala ya uchumi wa ndani na nje ya nchi pamoja na wawasilisha mada.