MAMA MARIAMU MWINYI AZUNGUMZA NA MTAALAMU WA MARADHI YA SARATANI KUTOKA HONG KONG CHINA

ZANZIBAR , 04 DISEMBA, 2024 MKE wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi amesema maradhi ya Saratani ni hatari na yanarejesha nyuma juhu...

Latest Post

MAMA MARIAMU MWINYI AZUNGUMZA NA MTAALAMU WA MARADHI YA SARATANI KUTOKA HONG KONG CHINA

Written By CCMdijitali on Wednesday, December 4, 2024 | December 04, 2024

ZANZIBAR,

04 DISEMBA, 2024




MKE wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Mama Mariam Mwinyi amesema maradhi ya Saratani ni hatari na yanarejesha nyuma juhudi za jamii na uchumi hata kusababisha umasikini kwa jamii kutokana na gharama kubwa za matibabu yake kwa wagonjwa wengi kutokuwa na uwezo wa kumudu matibabu.

Mama Mariam kwa huzuni ameyasema hayo Ofisini kwake Ikulu ya Migombani, Mkoa wa Mjini Magharibi alipozungumza na wageni kutoka Hong Kong, Dk. Jeremy Hon, Daktari na Mtaalamu wa maradhi ya Saratani akiambatana na Bi. Angel Hon wa Taasisi ya Belt and Road Creation Resources waliofika kumtemelea.

Mama Mariam Mwinyi ambae pia ni Msarifu na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF), aliwaeleza wageni hao jinsi wanavyofanyakazi na kuwa karibu na jamii kwa kuwashajihisha watu kuimarisha afya zao ili kujiepusha na maradhi yasiyoambukiza yakiwemo kisukari, presha na moyo.

Aidha, Mama Mariam aliueleza ugeni huo kwamba ZMBF katika kuisaidia jamii juu ya maradhi hatari ikiwemo Saratani taasisi yake mara kadhaa imekuwa na utaratibu wa kila baada ya miezi mitatu kuweka kambi za matibabu bure Unguja na Pemba kwa Mikoa yote kuisadia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na wakuu wa Mikoa kuwaalika wananchi kwaajili ya matibabu na uchunguzi wa afya zao.

Amesema, kambi hizo zimesaidia kugundulika kwa kesi nyingi zikiwemo Saratani za matiti zinazowasumbua kina mama wengi pamoja na maradhi mengine.

Mama Mariam amemualika Dk. Jeremy Hon kuangalia uwezekano wa kuja Zanzibar kushirikiana na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwani Serikali tayari imekamilisha hospitali 10 za Wilaya Unguja na Pemba na moja ya Mkoa pamoja na kuweka miundombinu imara na vifaa vya kisasa vya maabara.

Pia, Mama Mariam Mwinyi amewaeleza wageni hao jitihada za ZMBF kuishajihisha jamii kufanya mazoezi kwa kuungana nao mara kadha kwenye matembezi ya hiari ili kuimarisha afya zao sambamba na kuisajihisha jamii juu ya umuhimu wa lishe bora kwa mama wajawazito na watoto.

Akiuzungumzia mradi wa "Tumaini kit” unaozalisha taulo za kike kwa ajili ya hedhi salama kwa wasichana kupitia kiwanda chake kilichopo Mnara wa mbao, Mama Mariam Mwinyi aliwaeleza wageni wake hao lengo la mradi huo ni kutatua changamoto za hedhi kwa wanafunzi wa kike zinazorudisha nyuma maendeleo yao ya elimu kwa Unguja na Pemba.

Ameeleza kupitia mradi wa "Tumaini kit” umewasaidia wasichana wengi hasa wa vijijini kuhudhuria skuli na kufanya vizuri kwenye masomo yao ambao awali wengi waliacha kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutomudu gharama za kujikimu kila wanapopata ada za mwezi.

Halikadhalika, Mama Mariam Mwinyi amebainisha kuwa “Tumaini Initiative” umelenga kuzalisha taulo za kike zaidi ya 20,000 kwa mwaka na hadi sasa tayari ZMBF imefanikiwa kusambaza kwa wanafunzi na wasichana zaidi ya 7000 wa skuli za msingi na sekondari kwa Unguja na Pemba.

Katika hatua nyengine Mama Mariam Mwinyi aliueleza ugeni huo umuhimu wa kutumia mwani kiafya na kiuchumi na kusema kuwa taasisi yake ya ZMBF inawaungamkono wakulima wengi wa mwani amba oni kinamama kwa kuwasaidia mbinu, vifaa na kuwawezesha kuvuna mwani wenye ubora wa lengo la kujipatia soko imara la zao na bidhaa zinazotokana na mwani.

Kwa upande wao Dk. Jeremy Hon na Mrs Angel Hon wamepongeza juhudi za maendeleo na kazi nzuri inayofanywa na “Zanzibar Maisha Bora Foundation” ya kuhakikisha wasichana wa Zanzibar hasa wa vijijini wanakua salama muda wote wanapokuwa kwenye ada zao za kila mwezi.

Pia wameeleza shauku yao ya kutaka kuendeleza ushirikiano wao na Zanzibar hasa katika kubadilishana uzoefu kwenye sekta ya Afya ili kupunguza wimbi za maradhi ya Saratani yanayowasumbua wananchi wengi.


Naye, Ofisa Mkuu wa Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF), Fatma Fungo ameueleza ugeni huo kwamba taasisi hiyo mara nyingi imekua na programu za nje ya taasisi kwa lengo la kuifikia na kuwa karibu na jamii kwa kutoa elimu na kushajihisha jamii masuala mbalimbali ya Afya ikiwemo umuhimu wa hedhi salama kwa wanafunzi, wazazi, viongozi wa Serikali za mitaa, Wakuu wa Mikoa na Wilaya kwa maeneo yote wanayoyatembelea.


Aidha, amesema kupitia programu za kambi za matibabu tayari wamefanikiwa kuwafikia zaidi ya watu 17, 000 na kubaini kesi mbalimbali zinasowasumbua kiafya na kupatiwa matibabu kwa kushirikiana na Wizara ya Afya na mdaktari kutoka China, aidha, kwa kesi za ugawaji wa taulo za hedhi salama, amesema ZMBF imekua ikishirikiana kwa karibu na Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali.

Taasisi ya “Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF) iliasisiwa Julai mwaka 2021 na kuzinduliwa rasmi Febuari mwaka 2022.

“Zanzibar Maisha Bora Foundation” (ZMBF) inafanya kazi kwa karibu na tasisi za Serikali zikiwemo Mahakama ya Zanzibar, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Wizara ya Uchumi wa Buluu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee Wazee na watoto, Wizara ya Habari na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda.


IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR.










WAZIRI NDEJEMBI: WATHAMINI, HAKIKISHENI THAMANI HALISI INAJULIKANA

Na Eleuteri Mangi, Dodoma

 

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Deogratius Ndejembi amewataka Wathamini nchini kupunguza migogoro inayotokana na uthamini kwa kuhakikisha thamani halisi ya ardhi inayofanyiwa uthamini inajulikana. 

 

Mhe. Ndejembi amesema hayo baada ya kutunuku vyeti vya Taaluma ya Uthamini Wathamini waliohitimu mafunzo ya taaluma hiyo kwenye mahafali ya nne yaliyoenda sanjari na mkutano wa tano wa mwaka wa Bodi ya Usajili wa Wathamini (VRB) Desemba 4, 2024 jijini Dodoma.

 

Amesema, teknolojia inabadilika katika nyanja mbalimbali ikiwemo njia ya mawasiliano, namna ya kufanya kazi na biashara ambapo ameweka wazi kuwa, taaluma ya uthamini nayo haiko nyuma na inapaswa kuendana na mabadiliko hayo.

 

“Kama wathamini, ni muhimu mjikite katika matumizi ya zana za kidijitali zinazopatikana kwenu, kutoka kwa mifumo ya Kijiografia (GIS), Akili Bandia (AI), na Mifumo mbalimbali ya kidijitali. Teknolojia hizi zinawapa uwezo wa kufanya uthamini za ardhi na mali kwa usahihi zaidi na kwa ufanisi zaidi” amesema Waziri Ndejembi.

 

Waziri Ndejembi amewataka wathamini kuunganisha teknolojia katika kazi zao za kila siku kwa kuwa kunaboresha usahihi wa kazi za uthamini sambamba na kuimarisha uaminifu wa taaluma hiyo ili kukuza uwazi na haki, jambo ambalo alilolieleza linajenga imani miongoni mwa wawekezaji, taasisi za serikali, na jamii kwa ujumla. 

 

“Hivyo, nawaasa kila mmoja wenu kujitahidi kwenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia, kuwekeza katika maendeleo yenu ya kitaaluma na majukwaa mbalimbali ya kidijitali ambayo yanaweza kuboresha kazi zenu” amesema Waziri Ndejembi.

 

Kwa upande wake, Msajili wa Bodi ya Wathamini nchini Bw. Joseph Shewiyo amesema, kwa sasa kuna zaidi ya Wathamini 400 nchini ambapo kupitia mahafali hayo jumla ya wahitimu 34 wamehitimu.

 

Mkutano huo wa mwaka wa Bodi ya Usajili wa Uthamini (VRB) unaongozwa na Kaulimbiu “Mwelekeo wa Uthamini Tanzania; Kujumuisha Teknolojia, Uvumbuzi na Ustahimilivu wa Mazingira” kaulimbiu inayohimiza kuendelea kuzingatia mabadiliko ya kimataifa na maendeleo ya kiteknolojia kwa kuzingatia umuhimu wa uendelevu na ustahimilivu wa mazingira katika utendaji kazi wa wataaluma hao. 












WAZIRI KOMBO AHUTUBIA KATIKA CHUO CHA DIPLOMASIA CHA UAE



WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI BALOZI MAHMOUD THABIT KOMBO AKIHUTUBIA KATIKA CHUO CHA KIDIPLOMASIA CHA ANWAR GARGASH TAREHE 04 DESEMBA, 2024 JIJINI ABU DHABU IKIWA NI SEHEMU YA MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA UHUSIANO WA KIDIPLOMASIA KATI YA TANZANIA NA UAE


 Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo (Mb),ameshiriki maadhimisho ya miaka 50 ya uhusiano baina ya Tanzania na UAE yaliyoandaliwa na Chuo cha Diplomasia cha Anwar Gargash cha nchi hiyo.

 Akizungumza mbele ya wanafunzi na wahadhiri wa Chuo hicho, Mhe. Waziri Kombo alitoa rai ya kuendelea kuimarisha uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na UAE na kuweka misingi imara ya Kidiplomasia kwa vizazi vijavyo.

Kupitia mazungumzo yake chuoni hapo, Mhe. Waziri aliwasilisha salamu za pongezi kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu na Mtawala wa Abu Dhabi Mtukufu Sheikh Mohamed bin Zayed Al Nahyan na wananchi wa UAE kote duniani kwa kuadhimisha miaka 53 ya siku adhimu ya Taifa lao.

Mhe. Kombo amesema, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu zina historia ndefu ya urafiki na uhusiano tangu enzi za biashara za Ghuba ya Uajemi kupitia Bahari ya Hindi hadi mwambao wa Tanzania, kuanzia Zanzibar, Dar es Salaam hadi Mtwara.  
“Msingi imara uliowekwa na waasisi wa mataifa haya, marehemu Sheikh Zayed bin Sultan al Nahyan na hayati Mwalimu Julius Nyerere, Tanzania na UAE ziliimarisha uhusiano wa kidiplomasia mwaka 1974 baada ya kuungana kwa UAE mwaka 1971, “ alisema Balozi Kombo. 
Ameongeza kuwa uhusiano huo umeendelea kuwa wa kirafiki na wenye mshikamano tangu wakati huo na kwamba anaamini kuwa uhusiano huo utaimarika zaidi katika miaka mingi ijayo. 

 Mhe. Waziri Kombo ametumia mhadhara huo kunadi fursa za biashara, uwekezaji na Utalii zilizopo nchini na kuwaita wananchi wa UAE kuja nchini kuwekeza na hivyo kuzinufaisha pande mbili kupitia Diplomasia ya Uchumi .  
Akiongea kuhusu Ushirikiano na Chuo cha Diplomasia cha Anwar Gargash amesema Chuo hicho kina uhusiano na Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim ambao mwezi huu umetimiza mwaka mmoja tangu kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) iliyoanzisha uhusiano huo ambayo ilisainiwa mwezi Desemba 2023, wakati wa Mkutano wa COP28 uliofanyika Dubai. 

 “Kusainiwa kwa makubaliano hayo kunafanya kuwa chombo muhimu kinachochangia faida kubwa kwa ushirikiano uliopo, ikiwa ni pamoja na mafunzo ya muda mrefu na mfupi, kubadilishana uzoefu kati ya wakufunzi na wataalamu, kutoa mihadhara ya kidiplomasia, na kufanya utafiti wa pamoja kwenye maeneo kama utatuzi wa migogoro, diplomasia ya kiuchumi, na mengineyo,” alisema Balozi Kombo. 

 Pia alitumia mhadhara huo kukishukuru Chuo cha Diplomasia cha Anwar Gargash kwa kutoa nafasi za mafunzo kwa Maafisa wa Wizara kuhudhuria kozi fupi ya diplomasia katika Chuo hicho mwaka huu ambapo maafisa hao wanasubiri tarehe ya kuanza kozi na kuongeza kuwa ni matumaini yake kuwa Chuo hicho pia kitakuja nchini kujifunza uzoefu wa Tanzania.  
Alisema ni imani yake kuwa mafunzo hayo yatawajengea watumishi hao wa Wizara ujuzi wa vitendo na uzoefu unaohitajika katika kutekeleza majukumu yao na kukuza taaluma zao. 

Balozi Kombo yuko nchini UAE kuhudhuria majadiliano ya kwanza ya kisiasa na Kidiplomasia kati ya Tanzania na UAE ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na UAE ambapo pia ameshiriki katika maadhimisho ya miaka 53 ya Taifa la UAE yaliyofanyika Desemba 2, 2024.


Waziri Wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Mahmoud Thabit Kombo  katika Picha ya Pamoja alipomaliza Kuzungumza katika Chuo cha Kidiplomasia cha Anwar Gargash tarehe 04 Desemba, 2024 Jijini Abu Dhabu ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhusiano wa Kidiplomasia kati ya Tanzania na UAE 






KAULI MBIU YA MHADHARA HUO NI : KUTOKA MISINGI HADI MAJIRA YA BAADAYE: NUSU KARNE YA UHUSIANO KATI YA UAE NA TANZANIA. KUTOKA UHUSIANO WA KIHISTORIA HADI UHUSIANO WA KIDIPLOMASIA, KUELEKEA USHIRIKIANO WA KIUCHUMI KWA MANUFAA YA PAMOJA.


 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link