Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
Chama Cha Mapinduzi Zanzibar (CCM) kimempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi, kwa kutunukiwa Shahada ya Heshima ya Uzamivu na Chuo Kikuu cha Zanzibar.
Pongezi hizo zimetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo ya CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari katika ofisi za CCM, Kisiwandui, Zanzibar.
Mbeto alisema kuwa Chuo Kikuu cha Zanzibar kimemtunuku Shahada hiyo ya Heshima ya Uchumi kama ishara ya kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa Rais Dkt. Mwinyi katika uongozi wake, ambao umeacha alama ya kipekee na historia itakayokumbukwa wakati wote.
Alisisitiza kuwa heshima hii ni ushahidi wa mafanikio makubwa yaliyofikiwa Zanzibar, hasa katika kipindi kifupi cha uongozi wake wa miaka minne, ambapo uchumi wa Zanzibar umeimarika na maendeleo mbalimbali yamepatikana.
"Heshima hii inatokana na juhudi kubwa za Rais Dkt. Mwinyi katika kukuza uchumi, kuboresha huduma za kijamii, na kuleta mabadiliko chanya kwa wananchi wa Zanzibar. CCM Zanzibar ina furaha kubwa kumpongeza Rais Mwinyi kwa kutambuliwa na Chuo Kikuu cha Zanzibar kwa mchango wake mkubwa," alisema Khamis Mbeto.
Katibu Mbeto alitoa wito kwa wananchi wa Zanzibar kuendelea kumunga mkono Rais Dkt. Mwinyi na serikali yake katika juhudi zao za kukuza uchumi, kuboresha huduma za kijamii, na kuhakikisha Zanzibar inapata maendeleo ya kweli na endelevu.
Hafla ya kutunukiwa Shahada ya Heshima hiyo ilifanyika Disemba 5, mwaka 2024, katika Viwanja vya Chuo Kikuu cha Zanzibar, Tunguu, wakati wa Mahafali ya 22 ya Wahitimu wa mwaka 2024.
Katika hotuba yake, Rais Dkt. Mwinyi alishukuru Chuo Kikuu cha Zanzibar kwa kuthamini kazi anazozifanya kwa ajili ya maendeleo ya nchi.
Alieleza kuwa Shahada hiyo ni ishara ya mafanikio ya serikali yake na wananchi wa Zanzibar kwa ujumla, na itaongeza hamasa ya kufanya kazi zaidi katika kuleta maendeleo endelevu.
Rais Dkt. Mwinyi pia alisisitiza kuwa Shahada hiyo inawakilisha kazi nzuri inayofanywa na serikali anayoiongoza, na itaendelea kumhimiza katika kutimiza malengo ya maendeleo.
"Hii siyo mwisho wa safari, bali ni mwanzo wa hatua kubwa zaidi za maendeleo. Nitaienzi heshima hii na kuendelea kuwatumikia wananchi wangu kwa uwezo wangu wote," alisema Rais Dkt. Mwinyi.
MWISHO