Home » » WABUNGE WALIOPATA AJALI WATAJWA

WABUNGE WALIOPATA AJALI WATAJWA

Written By CCMdijitali on Monday, December 9, 2024 | December 09, 2024



December 8, 2024


DODOMA; 

WABUNGE wanne kati ya 17 waliokuwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Benjamin Mkapa wameruhusiwa baada ya afya zao kuimarika huku wengine wakiendelea kupatiwa matibabu.
Juzi watu 23, wakiwamo wabunge 17 walijeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuelekea Mombasa nchini Kenya kugongana na lori eneo la Mbande wilayani Kongwa Mkoa wa Dodoma.

Msafara huo ulikuwa unapitia Chalinze na Tanga kwenda Mombasa nchini Kenya kwa ajili ya kushiriki michezo ya 14 ya Mabunge ya Jumuiya ya Afrika Mashariki inayoshirikisha mabunge ya nchi saba yaliyoanza jana hadi Desemba 17, mwaka huu.

Akizungumzia hali za wabunge hao, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk Winnie Msangi alisema wabunge wanne wameruhusiwa baada ya afya zao kuimarika.

Alisema kuna wabunge ambao bado wamelazwa katika hospitali hiyo wakiendelea na matibabu ingawa wanaendelea vizuri.

“Kuna waheshimiwa (wabunge) wanne ambao afya zao zimeimarika, tumewaruhusu kurejea nyumbani na kuna wengine bado tunaendelea nao kuwapatia matibabu, lakini hali zao zinaendelea vizuri,” alisema.

Aliongeza: “Hatuna mbunge yeyote tuliyempa rufaa, kwani tunaweza kuwahudumia hapa hapa na hata hawa wanaoendelea na matibabu wako chini ya uangalizi wa madaktari ambao wanawahudumia kuhakikisha afya zao zinatengamaa na wanarejea nyumbani.”

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, George Katabazi aliwataja wabunge hao (majimbo) Florent Kyombo (Nkenge), Nicodemas Maganga (Mbogwe), Nicolas Ngassa( Igunga) na Jesca Msambatavangu (Iringa Mjini).
Wengine ambao ni wabunge wa viti maalumu ni Grace Tendega, Suma Fyandomo, Furaha Matonda, Zulfa Mmaka Omar, Juliana Shonza, Catherine Magige, Shamsia Mtamba na Mbunge wa Kuteuliwa, Abdul Yusuf.

Juzi Kamanda Katabazi alisema ajali hiyo ilitokea juzi saa 2:00 asubuhi katika barabara kuu ya Dodoma – Morogoro kwenye eneo la Mbande wilayani Kongwa ikihusisha basi la Kampuni ya Shabiby ambalo lilikuwa limebeba wabunge na maofisa wa bunge lililogongana na lori likitokea Morogoro kuelekea Dodoma.

Alisema ajali hiyo ilitokana na dereva wa basi lililowabeba wabunge kutochukua tahadhari wakati wa kuyapita magari mengine na baadaye kugonga tela na kutoka nje ya barabara na kusababisha majeruhi 23 na hakukuwa na kifo.




Share this article :
 
Support : #BegaKwaBegaNaMamaSamia | JAK | CCM Arusha
Copyright © 2011. CCM Dijitali - All Rights Reserved
Template Created by Creating Website Published by Jasper K
Proudly powered by Blogger
Link