Na: Nassoro Rashid - Mkingadc Habari
Mkuu wa wilaya ya Mkinga Mhe. Gilbert Sylvester Kalima Desemba 19, 2024 ameungana na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Katibu tawala pamoja na Afisa Maendeleo ya Jamii kuongoza ziara ya mafunzo ya uchumi wa buluu na uhifadhi wa bahari Zanzibar.
Ziara hiyo ya mafunzo ya siku 2 iliyoratibiwa na Shirika la Mwambao Coastal Network kwa kushirikiana na Serikali, imebeba lengo la kuimarisha mahusiano na ushirikiano mwema wa kuhakikisha agenda ya uchumi wa buluu na uhifadhi wa bahari inakuwa chachu ya kubadili uchumi wa Wananchi kwa kufahamika na kutekelezwa kwa vitendo.
Akizungumza katika ziara hiyo Mhe. Kalima amesema wamekuja Zanzibar kwa ajili ya kujifunza kwa vitendo ili kujipanga na kuangalia vipaumbele vya ziada vitakavyowawezesha kuvisimamia ili kuinua uchumi wa mkoa wa Tanga na wilaya zake kupitia eneo hilo la uchumi wa buluu.
"Sisi tumeanza kujifunza na tunawashukuru wenzetu wa Shirika la Mwambao kwa nafasi hii, kwa kweli tunaipongeza sana Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na hasa Rais wetu Mhe. Dkt Hussein Ali Mwinyi kwa uwekezaji mkubwa katika eneo hili la uchumi wa buluu, tutaitumia nafasi hii ili nasisi siku moja tuje kufanya vizuri kama mlivyofanikiwa hapa Zanzibar." Alisema Mhe. Kalima.
Sambamba na hayo amemuomba Katibu Tawala Mkoa wa Mjini Magharibi Ndugu Mohamed Ali Abdallah kuhusu suala la ushirikiano wa ulinzi na usalama maeneo ya bahari kwa mkoa wa Dar es Salaam na Mjini Magharibi (Zanzibar) kwamba, waongeze pia na mkoa wa Tanga na Pwani ili kuendelea kustawisha ulinzi na usalama katika maeneo yote.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi Zanzibar Ndugu Zahor Kassim El-Kharousy amesema wanathamini mchango wa mashirika katika kuitekeleza agenda ya uchumi wa buluu huku akisisitiza kuwa kwa sasa uwekezaji wa ukuzaji wa majongoo bahari umekuwa na tija na faida kubwa kutokana na kilo moja kuuzwa hadi dola 500, hivyo ametoa wito kuweka kipaumbele eneo hilo ili ikiwezekana fursa hiyo iweze kuwekezwa mkoa wa Tanga.
#Kaziiendelee